2393; Sifuri, Moja, Kumi, Mia na kuendelea…

Safari ya maili elfu moja huwa inaanza na hatua moja.
Hii ni kauli maarufu sana kwenye mafunzo ya hamasa na mafanikio.

Lakini imekuwa kauli rahisu kusema kuliko kuweka kwenye vitendo.
Watu wengi hawana subira wanapoianza safari ya mafanikio.

Wakiwaangalia waliofanikiwa, wanataka wawe kama wao walivyo sasa, hawazingatii kule ambapo watu hao wametoka na hatua walizopiga mpaka kufika walipofika.

Kila mtu huwa anaanzia sifuri, pale mtu anapokuwa chini kabisa. Japo wapo wanaoanzia hasi, mfano aliyekopa na kuwa kwenye deni kubwa ambalo anapaswa kulilipa.

Kutoka sifuri unaenda moja, hiyo ni hatua ambayo kwa matokeo unaweza kuona ni ndogo, lakini kwa mapinduzi ni kubwa.
Hakuna hatua ngumu kama kutoka sifuri kwenda moja.

Hata chombo cha moto, kukitoa kwenye kusimama kwenda kwenye mwendo inahitaji nguvu kubwa.
Nakumbula mashine za zamani za kusaga, ambazo zilikuwa zinawashwa kwa kuzungusha, mwanzo unakuwa mgumu, baadaye laini na kisha mashine inawaka.

Kadhalika kutoka kuwa hufanyi kitu mpaka kuanza kukifanya ni mapunduzi makubwa mno, hata kama hupati matokeo mazuri.

Kutoka moja unaenda kumi, hiyo ni hatua nyingine muhimu ambayo inazidi kujenga mizizi yako na kukupa kujiamini.

Kumi kwenda mia kunahitaji kazi zaidi, japo muda unaweza usiwe mrefu kama huko nyuma.
Mia kwenda elfu ndiyo hatua inayovunja ukomo mkubwa, hii inakuondoa kwenye mafanikio ya kawaida na kukufikisha kwenye mafanikio ya juu zaidi.

Elfu na kuendelea, hapo nguvu yako haina madhara sana, kinachohitajika ni mfumo mzuri wa kuhakikisha thamani inatolewa vizuri kwa wote.

Chini ya elfu moja (hasa kwa namba ya wateja), kila juhudi yako ina madhara ya moja kwa moja.
Lakini baada ya elfu moja, mfumo una nguvu zaidi kuliko juhudi zako binafsi.

Jua upo kwenye fungu lipi katika hayo, jisukume kuchukua hatua sahihi ili uweze kwenda mbali zaidi ya hapo ulipo sasa.
Huwezi kuruka hatua yoyote katika hizo, kwani kila moja ina funzo na mchango wake kwenye mafanikio yako.

Sifuri kwenda moja inakubadili kuwa mfanyaji.
Moja kwenda kumi inakutambulisha kwa unaowalenga.
Kumi mpaka 100 inaonyesha umejitoa kweli.
Mia mpaka elfu unatengeneza wafuasi wa kweli wanaokupa mafanikio.
Elfu na kuendelea ndiyo mafanikio makubwa kabisa.

Kocha.