Rafiki yangu mpendwa,
Hakuna kitu ambacho kimewapoteza wengi kwenye safari ya mafanikio kama kuhangaika na matokeo.

Watu wengi wanaohamasika kufanya kitu, huwa wanakimbilia kuangalia matokeo gani wanayapata. Na kama ni matokeo ambayo hawakutarajia basi huwa wanakata tamaa na kuachana na kitu hicho.

Hii ndiyo sababu inayopelekea wengi kukimbizana na kila aina ya fursa, lakini bado hawafanikiwi. Ni kwa sababu watu wanataka kuona matokeo ya haraka.

Chukua mfano wa mtu anayesikia kilimo cha tikiti kinalipa, anachukua hatua ya kwenda kulima, lakini msimu wa kwanza anapata hasara kubwa. Anasikia tena kilimo cha kitunguu kinalipa, anaenda kulima anapata hasara. Hajakaa sawa anasikia pilipili ndiyo inalipa zaidi, anaenda tena huko.

Ni nadra sana kufanya kitu kwa mara ya kwanza na kupata matokeo ambayo unayatarajia. Huwa inachukua muda katika kufanya, mwanzo ukiwa unashindwa na baadaye kuanza kujifunza na kupata matokeo mazuri.

Sasa kama wewe unachoangalia ni matokeo tu, kamwe huwezi kufanikiwa. Ni sawa na kutaka uanze darasa la kwanza na mwaka huo huo ufanye mtihani wa darasa la saba na kufaulu. Au mtu abebe ujauzito na ndani ya mwezi mmoja awe amejifungua mtoto.

Hakuna kitu kimeua ndoto za mafanikio ya wengi kama kuangalia matokeo. Pale lengo lako linapokuwa ni matokeo tu, ni kiashiria cha uhakika kwamba huwezi kufanikiwa.

Mwandishi Seth Godin kwenye kitabu chake kinachoitwa THE PRACTICE ameeleza kwa kina jinsi kuhangaika na matokeo kulivyo sumu kubwa.
Kwenye kitabu hicho ametoa mbadala wa kuangalia matokeo, ambao ni kupambana na mchakato.

Na hapo ndipo siri ya mafanikio ilipo rafiki yangu, achana na matokeo, pambana na mchakato.
Kwa chochote unachofanya, usiangalie nini unachopata, bali angalia nini unachotoa.
Usiangalie nini wengine wanakupa, angalia nini unawapa wengine.

Unapopambana na mchamato, maana yake unachukua hatua ambazo ni sahihi huku ukijifunza na kuwa bora zaidi.
Kadiri unavyoendelea na mchakato, ndivyo unavyojiweka kwenye nafasi nzuri ya kupata matokeo yaliyo bora zaidi.

Na kitendawili kizuri hapo ni hiki, unapohangaika na matokeo, huyapati. Lakini unapoachana na matokeo na kuhangaika na mchakato, unayapata matokeo mazuri sana.

Kwenye kitabu cha THE PRACTICE, Seth Godin ametushirikisha mambo 219 ya kuzingatia kwenye kutengeneza na kufuata mchakato sahihi katika kufikia mafanikio makubwa kwenye kile tunachofanya.

Seth anatuambia kwamba kila mmoja wetu tayari ni mbunifu, kinachohitajika ni kufanyia kazi mchakato sahihi ili kuweza kutoa ubunifu ulio ndani yako.

Karibu usome uchambuzi wa kitabu hiki cha THE PRACTICE, ujue jinsi ya kujenga mchakato utakaofanyia kazi ili uweze kufanya makubwa.

Pia tutakuwa na mjadala wa moja kwa moja wa kitabu hiki kupitia klabu ya usomaji wa vitabu ya SOMA VITABU TANZANIA.
Kwenye mjadala huo kila mtu anashirikisha yale aliyojifunza na namna anavyoyafanyia kazi kwenye maisha yake.
Pia unapata nafasi ya kuuliza maswali na kupata ufafanuzi kwenye mambo mbalimbali ambayo hukuyaelewa.

Kusoma uchambuzi wa kitabu hiki cha THE PRACTICE pamoja na kupata nafasi ya kushiriki mjadala wa moja kwa moja, tuma ujumbe kwa telegram kwenda namba 0717 396 253 wenye majina yako, namba ya simu na maneno SOMA VITABU.

Usikubali matokeo yaendelee kuwa kikwazo kwako kufanikiwa. Badala yake jifunze jinsi ya kujijengea mchakato sahihi utakaoufanyia kazi na upate matokeo sahihi kwa mafanikio yako.

Karibu usome uchambuzi na kushiriki mjadala, utoke na mambo ya kwenda kufanyia kazi ili maisha yako yawe bora zaidi.

Rafiki yako anayekupenda sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani.
www.somavitabu.co.tz