2397; Mambo ya kuzingatia unapokuwa juu…
Kila mtu anapenda kwenda juu, kufika kwenye kilele cha juu kabisa cha mafanikio.
Lakini wengi huangalia upande mmoja tu wa kuwa juu, upande wa mazuri.
Kuwa juu kuna upande wa mabaya yake, ambao unaambatana na changamoto mbalimbali.
Ipo kauli inayosema kadiri unavyokwenda juu, ndivyo unavyoanguka kwa kishindo kikubwa.
Ikimaanisha unapokuwa umekwenda juu sana, anguko lako huwa linakuwa kubwa zaidi.
Kauli nyingine inasema kadiri nyani anavyokwenda juu, ndivyo mkia wake unavyoonekana zaidi.
Ikimaanisha mtu anavyokwenda ngazi za juu, madhaifu yake yanaonekana zaidi kuliko alivyokuwa chini.
Kauli hizo mbili zinapaswa kutupa tahadhari za kufuata ili tunapokuwa juu tuepuke upande mbaya.
Haya ni mambo ya kuzingatia pale unapokuwa juu.
- Fanya kila kitu kwa uaminifu na uadilifu mkubwa. Usifanye chochote ambacho hungependa kiandikwe kwenye kurasa za mbele za magazeti.
-
Tambua kadiri unavyokwenda juu ndivyo unavyokuwa huna siri. Hivyo usiwe na siri nyingi unazotaka kuzificha.
-
Jijengee kinga za anguko hata kama huoni linaweza kuja. Hakikisha hata anguko litakapokuja halitakuwa la kishindo kikubwa na pia uwe na pa kuanzia baada ya anguko.
-
Usiwe na kiburi na kuona tayari umeshajua kiasi gani, hata kama uko juu kiasi gani, kuna mengi bado huyajui. Endelea kuwa mnyenyekevu na kujifunza.
-
Epuka sana umaarufu kadiri unavyoweza. Kadiri unavyokwenda juu, taarifa zako zitawafikia wengi. Waache wabaki na taarifa zako lakini wasikujue wewe. Umaarufu ni mzigo mkubwa kwenye mafanikio, kwani unakuwa shambulio la kila mtu.
-
Kuwa tayari kusikia usiyotaka kusikia. Kadiri unavyokwenda juu, ndivyo unavyozungukwa na watu wanaokuambia ndiyo kwenye kile kitu, wanaotaka kukufurahisha na hivyo kukuambia unachotaka kusikia. Tengeneza watu watakaokuambia ukweli ambao ni vigumu kuusikia unapokuwa juu.
-
Tengeneza timu ya watu wanaokusaidia kadiri unavyokwenda juu.
-
Mara moja moja jikumbushe maisha ya chini kwa vitendo, itakufanya uwe mnyenyekevu.
-
Usijishikize na kile ulichonacho au nafasi uliyonayo, juwa wakati wowote unaweza kuvipoteza. Unapaswa kubaki imara hata ukipoteza kila kitu.
-
Toa kwa ajili ya wengine, umetumika kama njia ya kufika juu ili uwasaidie wengine nao wafike juu pia. Usifike juu kisha ukawazuia wengine ili wasifike. Hutabaki juu kwa kuwashikilia wengine chini. Utabaki juu kwa kuwasaidia wengi ziadi nao kufika juu kama wewe.
Zingatia haya unapokuwa juu, utaepuka kuanguka vibaya na hata utakapoanguka, utakuwa na pa kuanzia ili kurudi tena juu.
Kocha.