Rafiki yangu mpendwa,
Nionyeshe tabia zako na nitaweza kutabiri kwa kiwango kikubwa utakuwa wapi miaka 5, 10 na hata 20 ijayo.

Watu wasiofanikiwa huwa wanalalamikia karibu kila kitu kama kimwazo kwa mafanikio yao, isipokuwa kitu kimoja tu, tabia zao.

Na tabia ndiyo zenye nguvu kubwa ya kujenga au kubomoa mafanikio yako.

Mafanikio au kushindwa siyo tukio. Hakuna mtu anaamka siku moja na kujikuta amefanikiwa au ameshindwa.

Mafanikio au kushindwa ni mchakato, ambao unatengeneza kwa muda mrefu. Kitu chochote ambacho kinatengenezwa kwa mchakato kinaathiriwa sana na tabia ambazo mtu anakuwa nazo.

Unajionea hapo jinsi tabia zako zilivyo na athari kwenye mafanikio yako.
Ukivyo leo ni matokeo ya tabia ulizokuwa nazo huko nyuma.
Na kama utaendelea na tabia hizo, utaendelea kupata matokeo kama unayopata sasa.

Ndiyo maana nakuambia nikizijua tabia zako, najua wapi utaishia, siyo muujiza, ukipanda mbegu ya haragwe hushangai ukiota mche wa haragwe.
Kadhalika matokeo unayoona kwenye maisha yako, mbegu yake ni tabia ulizonazo.

Kama hujapata kile unachotaka au kufika unakotaka, kuna tabia ulizonazo sasa ambazo ni kikwazo kwako.
Bila ya kuvunja tabia hizo, itakuwa vigumu sana kwako kufanikiwa.

Kwa uzoefu wangu wa kufanya kazi na watu mbalimbali wanaotaka kufanikiwa zaidi, nimeziona tabia zifuatazo kuwa kikwazo kwa mafanikio. Uvivu, uzembe, ulevi, uzinzi, umbeya, wizi, dharau, kiburi, ujuaji, hasira, kutokujifunza, kukosa uaminifu, tamaa na kutokujali wengine.

Kama una tabia yoyote kati ya hizo, unapaswa kuivunja mara moja ili isiwe kikwazo kwa mafanikio yako.
Hata ikitokea umefanikiwa ukiwa na tabia hizo mbaya, anguko lako linakuwa kubwa na kinaloumiza zaidi.

Ili kuondokana na tabia mbaya zinazokuwa kikwazo kwa mafanikio yako, zingatia haya;

I. Badili mtazamo wako.

Mtazamo ulio nao ndiyo mzizi wa tabia ulizonazo. Huwezi kubadili tabia bila kubadili mtazamo. Ni sawa na kukata matawi na kuacha shina.

Mtazamo ni ile imani unayokuwa nayo kwako mwenyewe, ni vile unavyojiona ndani yako.

Kwa tabia mbovu ulizonazo, una mtazamo fulani unaozizalisha.
Wengi wana mtazamo wa kurithi, kwamba tabia hizo wamerithi kutoka kwa wazazi wako.

Unakuta mtu ni mlevi na anakuambia kwetu tuna asili ya ulevi. Au ana hasira asizoweza kudhibiti na kusema sisi huwa tuna hasira sana.

Mitazamo ya aina hii inazihalalisha tabia mbaya na kuzifanya zionekane ni sugu.

Vunja kabisa kila mtazamo ulionao unaohalalisha tabia zako mbaya.
Tambua wewe ndiyo mwenye nguvu na mamlaka ya kujenga mtazamo na maisha yako kwa ujumla.

Usijichukulie kama mtu mwenye hatia na dhaifu, bali jichukulie kama mtu mwenye mamlaka ya kuyabadili maisha yako.

Jua unaweza kuwa vile unavyotaka na haijalishi umetokea kwenye mazingira gani, una nguvu ya kuyabadili maisha yako.

Jenga mtazamo sahihi na utaweza kujenga tabia sahihi.

II. Tengeneza tabia mbadala.

Kama unataka kuvunja tabia mbaya, hakikisha unajenga tabia nyingine nzuri ya kuchukua nafasi ya tabia hiyo.

Ukiondoa tabia na kuacha uwazi, utajikuta unarudi kwenye tabia hiyo au tabia nyingine mbaya.

Kama unataka kuacha ulevi, unapaswa kuutumia ule muda uliokuwa unalewa kufanya mambo mengine yanayokuweka bize.
Inaweza kuwa kujifunza au kushirikiana na wengine wanaofanya mambo mazuri.

Asili haipendi utupu, ukivunja tabia na kubaki na muda ambao ni tupu, unatoa nafasi kwa tabia hiyo au nyingine kuchukua nafasi hiyo.

III. Badili mazingira.

Huwezi kuvunja tabia kwa kuwa kwenye mazingira yale yale yanayochochea tabia hiyo.
Badili mazingira yako ili uwe mbali kabisa na tabia unauotaka kuivunja.

Epuka makundi ya watu walio na tabia unayotaka kuvunja, maana wale unaokuwa nao wana ushawishi mkubwa kwako.

Kama unataka kuacha ulevi, achana na marafiki zako ambao ni walevi. Na usiende kufanyia vikao eneo la baa au kuwa na pombe ndani kwako.

Usijidanganye kwamba wewe ni imara na unaweza kukataa. Mazingira na wanaokuzunguka wana ushawishi mkubwa sana kwako.

Jipunguzie vishawishi kwa kubadili mazingira yanayochochea tabia unayotaka kuvunja.

IV. Vunja kila aina ya daraja.

Kuna daraja kati yako na tabia mbaya ambayo ni kikwazo kwako, vunja madaraja yote.

Kama umekuwa na tabia ya uzinzi, una michepuko, vunja madaraja yote na michepuko hiyo.  Kosana nao kiasi kwamba hata siku ukirudi kuwaomba msamaha hawawezi kukuelewa kabisa.

Kuvunja tabia ni vita, unachotaka ni ushindi, hivyo kila silaha inayoweza kukusaidia, itumie.

V. Tengeneza uwajibikaji.

Peke yako ni rahisi kurudi nyuma. Unapokuwa na mtu wa kukuwajibisha unajisukuma zaidi kwa sababu unajua kurudi nyuma kutakugharimu.

Tafuta mtu unayemheshimu na mwahidi nia yako ya kuvunja tabia mbaya uliyonayo.
Mweleze hatua unazokwenda kuchukua.
Kisha mpe adhambu ambayo atakupatia unapokwenda kinyume na ulivyoahidi.

Inaweza kuwa ni umlipe kiasi kikubwa cha fedha ambacho kitakuuma sana.
Au inaweza kuwa ni yeye kukudhalilisha kwa namna fulani.

Jenga uwajibikaji ambao unajua usipofanya kuna kitu utapoteza na hilo litakusukuna kufanya.

VI. Jua na kuliishi kusudi lako.

Kuhangaika na tabia mbovu ni kiashiria kwamba bado hujalijua kusudi la maisha yako.
Maana unapolijua kusudi, unagundua jinsi muda ulivyo mfupi.
Muda wako wote unaupeleka kwenye kuliishi kusudi lako na unakuwa huna muda wa kupoteza.

Kaa chini na ujitafakari kwa kina mpaka ulijue kusudi lako, kisha tumia kila dakika ya maisha yako yaliyosalia hapa duniani kuliishi kusudi lako.

Kadiri kusudi lako linavyokuwa kubwa, ndivyo unavyosukumwa kuachana na tabia mbaya zinazokuwa kikwazo kwa kusudi ulilonalo.

VII. Kuwa na ndoto kubwa.

Ndoto kubwa kabisa,  ndoto zinazokutisha wewe na wengine ni kinga dhidi ya tabia mbovu.

Mfano kama ndoto yako ni kuwa bilionea, hutapata muda wa kulewa kila siku. Ndoto hiyo itanyonya muda wako wote, mpaka utakosa muda wa kupumzika au kuwa na wale wa karibu.

Kama tabia mbaya zinakusumbua, chukua lengo lolote ulilonalo sasa, lizidishe mara kumi na waahidi watu kwamba lazima utafikia lengo hilo.

Waambie watu wazi kabisa kwamba utafikia lengo lako kubwa.
Unajua nini kitatokea, watakukatalia, watakupinga, watakudhihaki na kila  mara watakapokuona ukifanya tabia zisizo sahihi, watakukebehi.

Hayo tu yanayosha kukuondoa kwenye tabia mbaya na ambazo ni kikwazo na kukuweka kwenye tabia nzuri za kukufikisha kwenye ndoto zako kubwa.

VIII. Ambatana na watu sahihi.

Unapaswa kuambatana na watu sahihi, watu wenye tabia njema na watu ambao utajisikia aibu sana pale watakapojua tabia zako mbaya.

Wale wanaokuzunguka wana ushawishi sana kwenye tabia unazokuwa nazo, hivyo wachague kwa usahihi.

Pia kuwa na menta na/au kocha anayekusaidia kuondoka kwenye tabia mbaya na kujenga tabia nzuri kwa mafanikio yako.

IX. Yaonee huruma maisha yako.

Kwenye kitabu cha Follow Your Heart mwandishi anasema maisha yakiwa rahisi, huwa tunatafuta njia ya kuyafanya kuwa magumu zaidi.

Na hilo liko wazi, tabia nyingi mbaya na zinazotukwamisha, huwa tunazijenga pale maisha yanapokuwa rahisi.

Mtu anapokuwa hana fedha, anakuwa haba mambo mengi, lakini akizipata fedha ndiyo kila kitu kibaya kinamhusu, ulevi, uzinzi, dharau, kiburi n.k.

Yaonee huruma maisha yako, usitake kuyafanya yawe magumu kulikl yalivyo.

X. Usiwe mbishi.

Huwa ipo kauli kwamba mtu mmoja alikuambia una tatizo, huenda yeye ndiye mwenye tatizo.
Watu watatu wakikuambia una tatizo, huenda kuna njama (Conspiracy) wanafanya dhidi yako.
Lakini watu 10 wakikuambia una tatizo, basi ni kweli una tatizo.

Tabia mbovu zimekuwa kikwazo kwa wengi kwa sababu ya ubishi. Wengi hawapendi kukiri kwamba tabia walizonazo ndiyo kikwazo kwao.

Na hupenda kutumia kauli za kuwafariji, wakitaja watu wengine waliofanikiwa licha ya kuwa na tabia kama zao.

Rafiki, hili siyo swala la kujilinganisha na wengine, ni swala la kujitafakari wewe mwenyewe na kuona tabia ulizonazo zimekuwa na mchango au vikwazo gani kwako.
Hata kama kwa wengine zina manufaa, kama kwako hazina manufaa achana nazo.

Zingatia haya uliyojifunza hapa ili uweze kubomoa tabia mbaya na ambazo ni kikwazo kwako.
Kama unahitaji msaada wa kocha katika kuvunja tabia yoyote mbaya uliyonayo, karibu tufanye kazi pamoja. Wasiliana na mimi kwa namba 0717 396 253.

Pia pata na usome kitabu cha TABIA ZA KITAJIRI, kitabu kinachokufundisha tabia mpya za kitajiri unazopaswa kuziishi kwenye maisha yako ili kufanikiwa.
Kitabu kina imani 17 potofu unazopaswa kuzivunja kwenye maisha yako. Kukipata wasiliana na namba 0717 396 253.

Rafiki yako anayekupenda sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani,
www.somavitabu.co.tz