2406; Unachoona na usichoona…

Umewahi kuangalia tangazo au mafunzo ya kitu kwenye tv au mtandaoni, ukatoka na kwenda kujaribu kufanya kama ulivyojifunza?

Kama ndiyo mara ya kwanza kufanya kitu hicho, utakuwa ulipata matokeo ya tofuati kabisa na uliyoyaona, hata kama umefanya kila ulichoelekezwa.

Hiyo ni kwa sababu unachoona ni matokeo ya mwisho baada ya majaribio mengi.
Kuna kikubwa ambacho huoni, ambayo ni majaribio ya muda mrefu ili kuweza kuzalisha matokeo mazuri mwishoni.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye michezo mbalimbali.
Wachezaji huwa wanatumia muda mwingi kufanya mazoezi kuliko muda wanaotumia kwenye michezo husika.

Mcheza mpira atacheza uwanjani dakika 90, lakini kwa siku atafanya mazoezi kwa zaidi ya masaa matatu.
Wewe unaona dakika 90, huyaoni masaa mengi ambayo yamefanya maandalizi ya dakika 90.

Kadhalika kwenye mafanikio, unawaona tu watu wakiwa juu, wakiwa wanafanya makubwa.
Usichoona ni magumu waliyopitia, mapambano waliyokabiliana nayo na kushindwa ambapo wamepitia.

Upo usemi wa Kiswahili unaosema usione vyaelea, vimeundwa.
Chochote unachoona kwa nje na ukakifurahia au kukitamani, jua kuna kikubwa nyuma yake ambacho hukioni.

Mara zote zingatia yale usiyoona ili uweze kujipanga vizuri na kupata kile unachotaka.

Unaona matokeo, huoni juhudi.
Unapoyaona matokeo unaona ni rahisi kuyafikia, lakini siyo rahisi kama unavyodhani.

Kukadiria kitu vibaya kwa kuyaangalia matokeo ni chanzo cha wengi kupata anguko kwenye yale wanayofanya.
Usichukulie chochote poa, jua kuna uwekezaji mkubwa umefanyika.

Kocha.