2413; Ubaya ni kusimama…

Kitu pekee unachohitaji kwenye maisha ni kuwa kwenye mwendo.

Haijalishi unakwenda kwa kasi kiasi gani, muhimu ni kuwa kwenye mwendo.

Jambo baya kabisa kwenye maisha ni kusimama.

Kwa sababu dunia haisimami, hivyo unaposimama unakuwa umechagua kurudi nyuma.

Unapaswa kujikumbusha kwamba chochote cha maana unachotaka kwenye maisha yako, kitahitaji muda mrefu kuliko unavyotegemea.

Ni asili yetu binadamu kutaka mambo yaende kama tunavyopanga, kutaka yawe haraka kama tunavyotegemea.

Lakini dunia haiendi kwa kuangalia matakwa yetu, dunia inaenda kwa namna yake yenyewe.

Wajibu wetu ni kuchukua hatua sahihi na muhimu katika kufanyia kazi kile kilicho muhimu kwako.

Kaa kwenye njia yako na songa mbele, usihangaike na njia za wengine na fanya chochote ili tu kusonga mbele.

Na kama Martin Luther King alivyowahi kusema, kama huwezi kuruka basi kimbia, kama huwezi kukimbia basi tembea na kama huwezi kutembea basi tambaa.
Fanya chochote ili tu kusonga mbele.

Na huo ndiyo wajibu wako, kusonga mbele na siyo kusimama pale ulipo sasa.
Maana kusimama ni kuchagua kurudi nyuma.

Kocha.