2425; Yaweke maoni sehemu sahihi…

Huwa kuna kauli kali sana kuhusu maoni ambayo inasema; maoni ni kama tundu la choo, kila mtu analo na ya wengi yananuka.

Huwa tunayapa maoni ya watu uzito ambao hayastahili.
Tunaona kama maoni hayo ndiyo ukweli tunaopaswa kuufuata.

Lakini unapaswa kujua maoni ni maoni tu, kila mtu ana yake na siyo rahisi yakaendana na kile unachotaka wewe.

Na tatizo la maoni ni watu huwa wanakuwa tayari kukupa maoni yao bure, kabla hata hujawaomba.

Na ubaya ni wanakupa maoni kulingana na mtazamo wao, ambao ni tofauti kabisa na mtazamo ulionao wewe.

Unachohitaji wewe ni kujua ukweli ulipo na kuusimamia huo.
Maoni ni mengi, ukikimbizana nayo yatakupoteza vibaya sana.

Yaweke maoni sehemu sahihi, ambayo ni siyo muhimu sana.
Usibadili mambo yako makubwa kwa sababu ya maoni tu ya watu.

Maamuzi yoyote unayofanya yanapaswa kuongozwa na ukweli, siyo maoni.

Kocha.