2457; Matumizi Ya Teknolojia Mpya.
Kila wakati huwa kuna teknolojia mpya ambazo zinavumbuliwa.
Teknolojia hizo huwa zina nguvu ya kuleta mabadiliko makubwa na hivyo kuonekana ni fursa nzuri.
Watu wengi hukimbizana na teknolojia hizo mwanzoni, ili kuzihodhi wakiona ndiyo namna ya kunufaika nazo.
Lakini mwisho wa siku wanaofaidika sana siyo wale wanaohidhi teknolojia hizo, bali wale wanaozitumia kuboresha kile wanachofanya.
Teknolojia mpya ni njia na siyo mwisho wa safari yenyewe.
Kama huna unapoenda, teknolojia mpya haiwezi kuwa na msaada kwako.
Chukua mfano wa intaneti, wakati intaneti inaanza kuwa wazi kwa wote, katikati ya miaka ya 90, makampuni mengi ya intaneti yalianzishwa.
Mengi ya makampuni hayo hayakuwa na thamani yoyote, ila tu kwa sababu intaneti ilikuwa kitu kipya na ambacho watu walitegemea kitaleta mapinduzi makubwa.
Makampuni yalianzishwa mengi na kwa urahisi mwishoni mwa miaka ya 90, lakini anguko kubwa lilitokea na mengi ya makampuni hayo yalikufa kabisa.
Lakini yapo makampuni yaliyovuka anguko hilo yakiwa imara na mpaka leo ni makampuni makubwa.
Moja ya makampuni hayo ni Amazon, ambayo ilitumia intaneti kama njia na siyo kama fursa.
Lengo la Amazon tangu inaanzishwa limekuwa kuwarahisishia watu kupata mahitaji yao kwa kutumia mtandao wa intaneti.
Na msingi wake mkubwa umekuwa ni kutoa huduma bora kabisa na ya haraka kwa mteja.
Hivyo ndiyo vimeiwezesha kampuni ya Amazon kufanikiwa sana.
Kutumia mtandao wa intaneti ni njia tu, lakini nyuma yake kuna thamani kubwa ambayo inatolewa.
Ndiyo kinachoendelea sasa kwenye cryptocurrency au kama inavyoitwa kwa urahisi fedha za kidijitali.
Wengi wanahangaika nazo kama fursa na ndiyo maana thamani yake inapanda na kushuka kwa muda mfupi sana.
Lakini watakaonufaika kwa kipindi kirefu na teknolojia hii mpya, ni wale wanaoitumia kuboresha kile ambacho tayari wanafanya, ambao tayari kuna thamani wanazalisha na wanatumia teknolojia hiyo kutoa thamani hiyo kwa ubora zaidi.
Wengi sana wataendelea kuhangaika na teknolojia mpya zitakazoendelea kuja kila siku.
Ila watakaonufaika hasa watakuwa ni wale wanaozitumia kuboresha kile ambacho tayari wanafanya au thamani ambayo wanapanga kutoa.
Hatua ya kuchukua;
Kama kuna teknolojia mpya umeiona ni fursa, jiulize unawezaje kuitumia kufanya kwa ubora zaidi kile ambacho tayari unafanya.
Usikimbizane tu na teknolojia kama ndiyo fursa, hilo litakuondoa kwenye ndito zako kubwa.
Baki kwenye ndoto zako kubwa unazotaka kufikia na kwa kila teknolojia mpya inayokuja, jiulize inakusaidiaje kufikia ndoto hizo.
Kama haina msaada kwenye ndoto zako, usijisikie vibaya kuachana nayo, hata kama kila mtu anahangaika nayo.
Tafakari;
Teknolojia mpya siyo fursa, bali ni njia ya kuwezesha fursa mbalimbali kufanyika kwa ubora zaidi.
Wanaonufaika na teknolojia siyo wanaohangaika nazo, bali wanaozitumia kufanya kwa ubora zaidi kile ambacho tayari wanafanya.
Kocha.
Asante Sana kocha.
LikeLike
Karibu.
LikeLike