2458; Hatari sahihi kuchukua.

Kwenye maisha, hakuna kitu chochote ambacho kina uhakika wa asilimia 100.
Kila kitu huwa kina kiwango chake cha hatari.

Kitu kinapokuwa kipya hatari yake ni kubwa kwa sababu mtu unakuwa huna uzoefu.
Lakini kitu ambacho kimezoeleka hatari yake ni ndogo, kwa kuwa tayari mtu unakuwa na uzoefu.

Ni uzoefu ambao unatupa upofu kwenye hatari ndiyo umekuwa kikwazo kwa mafanikio ya wengi.

Mfano mtu aliyeajiriwa na ambaye mshahara unaingia kila mwezi, ataona hiyo ni njia salama kuliko kufanya biashara.
Lakini siyo kwamba haina hatari, ila mazoea yamempa upofu kwenye hatari iliyopo.
Ajira ina hatari ya ukomo wa kipato, hatari ya kufukuzwa na hatari ya ukomo wa muda kwamba lazima ustaafu.

Hivyo kwenye safari ya mafanikio, kama unataka kuyapata mafanikio makubwa, lazima uweze kupima hatari kwenye mambo mbalimbali na kujua yapi sahihi kwako kufanyia kazi ili kufanikiwa.

Na hatari sahihi kwako zina sifa tatu.

Moja ni uwezekano wa kushinda ni mkubwa kuliko wa kushindwa.
Ukichukua hatari ambayo uwezekano wa kushinda na kushindwa unalingana, hiyo ni kamari.

Mbili ni faida inayoweza kupatikana ni kubwa sana kuliko hasara inayoweza kupatikana.
Kama ukishinda, umeshinda kweli na kama ukishindwa, ni kidogo.

Tatu ni kushindwa hakuwi kifo. Yaani kama utashindwa, haiwi ndiyo mwisho ambapo huwezi kujaribu tena wakati mwingine. Unapaswa kuwa na nafasi ya kufanya tena wakati mwingine hata kama sasa umeshindwa.

Hatua za kuchukua;
Ni kitu gani ambacho umekuwa unatamani sana kufanya ila kila mara unaahirisha kwa sababu ya hatari unayoiona na kuihofia?
Leo kaa chini na ukokotoe kabisa kiwango cha hatari kwa kutumia sifa hizo tatu.
Kama zote zipo, basi anza mara moja kufanya kitu hicho, hata kama utashindwa, utakuwa umejifunza mengi kuliko kutokufanya kabisa.

Tafakari;
Kutaka usalama na uhakika kumekuwa chanzo cha wengi kujiweka kwenye magereza ambayo yamekuwa kikwazo kwa mafanikio yao.
Ondoka kwenye hayo magereza, kokotoa hatari zinazokukabili na chukua hatua sahihi.

Kocha.