2461; Unachojua kinatosha kuanza.

Kama kuna kitu chochote unachotaka kufanya, lakini unajiambia bado hujajua kiasi cha kutosha kuanza jua unajidanganya.

Kitendo cha kujua unataka kufanya kitu fulani, ni kiashiria kwamba unajua kiasi cha kutosha kuanza.
Kama ungekuwa hujui kwa kiasi hicho, usingeweza kupata wazo la kufanya kitu hicho.

Ni kweli kwamba unayojua ni kama tone tu kwenye bahari ya mengi unayopaswa kujua.
Lakini huwezi kujua kila kitu unachopaswa kujua.
Unapaswa kujua kiasi cha kutosha kuanza.
Ambacho tayari umeshakuwa nacho.

Kujua zaidi kabla hujaanza inaweza kuwa hata kikwazo kwako usianze. Kwani kadiri unavyojua ndivyo unajiona hujawa tayari kuanza.

Wakati mwingine kutokujua sana kuna manufaa, kwani unakuwa na kujiamini kwa ujinga, kitu ambacho kinakupa nguvu ya kufanya kitu kwa kutokujua kwamba hakiwezekani.

Wengi wa waliofanya makubwa, hawakujua kwamba haiwezekani. Siyo kwamba walijua haiwezekani ila wakajiambia wataweza, wao hawakujua kabisa kwamba ni kitu kisichowezekana.

Wakati Hendry Ford anawaambia mainjinia wake watengeneze injini ya piston 6, hakujua ni kitu kisichowezekana kisayansi. Mainjinia wake walimwambia hicho ni kitu kisichowezekana kifizikia. Yeye hakuwa anaelewa wanaongelea kitu gani, aliwaambia anataka injini na akaipata.

Wakati Wright Brothers wanatengeneza ndege ya kwanza, wanafizikia walishafikia hitimisho kwamba kurusha chombo angani ni kitu ambacho hakiwezekani kwa angalau miaka 100 mbeleni. Wao walikuwa wanajua kanuni zote za fizikia na nini kinawezekana na kisichowezekana.
Wright Brothers hawakujua kanuni hizo, walijua wanataka kurusha chombo hewani na hilo ndilo walilofanyia kazi na wakafanikiwa.

Huhitaji kujua zaidi ya unachojua sasa ndiyo uanze. Wewe anza, mengine usiyojua utajifunza mbele ya safari.

Hatua ya kuchukua;
Jiulize ni mambo gani umekuwa unataka kuanza kufanya, lakini unajiambia bado hujajua vya kutosha.
Chagua moja muhimu leo na anza mara moja kufanya, ukijua tayari unajua vya kutosha na kujua zaidi kutakuwa kikwazo kwako.
Anza na mengine utajifunza mbele ya safari.

Tafakari;
Kutokujua kisichowezekana ni bahati kubwa, kwani hofu hazitakuwa kikwazo kwako. Jenga tabia ya kuanza kufanya yale muhimu kabla hujajua sana kwa undani ili unapoyajua yasikupe hofu ya kuanza.

Kocha.