2465; Hudanganywi ila unajidanganya.
Huwa tunalalamika kwamba watu wengine wametudanganya kwenye mambo mbalimbali.
Wakatufanya tuamini kwa namna fulani ambayo siyo sahihi.
Unaweza kuona uko sawa kwenye hilo, lakini ukiangalia kwa undani, utaona wazi haupo sawa.
Watu huwa hawakudanganyi, ila umekuwa unajidanganya mwenyewe.
Twende taratibu hapa maana inahitaji utulivu na umakini mkubwa kuelewa dhana hii.
Katika kila kitu ambacho mtu anakuambia, ukweli na uongo huwa vinaonekana dhahiri kabisa.
Tatizo linakuja kwamba wewe unachagua unataka kuona nini.
Kwa kawaida, sisi binadamu huwa tunaona kile tunachotaka kuona na kusikia kile tunachotaka kusikia.
Mambo yanaweza kuwa mengi, lakini sisi tunachagua kile kinachoendana na tunachotaka.
Tatizo hili limekuwepo miaka yote, maana ni moja ya madhaifu yetu binadamu kwenye kufanya maamuzi. Lakini kwenye zama hizi tatizo limekuwa kubwa, kwa sababu mitandao ya kijamii inazidisha hili.
Mitandao ya kijamii huwa inaangalia tabia yako ni vitu gani unafuatilia zaidi na kukuletea vitu vya aina hiyo zaidi.
Sasa wewe unaweza kuona hivyo pekee ndivyo vilivyopo, kumbe siyo.
Tukirudi kwenye kujidanganya, kama unataka sana kitu fulani, basi utaona ushahidi unaoendana na wewe kukitaka.
Kunaweza kuwa na ushahidi wa wazi unaopingana na matakwa yako, lakini utaupuuza na kuchukua ule unaoendana na unachotaka.
Kadhalika kama kuna kitu hutaki, utachukua zaidi ushahidi unaoendana na wewe kutokukitaka kuliko ushahidi unaopingana na wewe.
Taarifa zote ziko wazi ni wewe unayeamua uchukue zipi.
Hivyo hata kwenye kudanganywa, hakuna anayekudanganya, bali wewe mwenyewe unajidanganya.
Hata kama mtu anakuja kwako na uongo ambao ameuweka kama ukweli, kuna viashiria vya wazi kwamba ni uongo. Kama unataka sana kitu hicho kiwe kweli, utapuuza viashiria vinavyoonyesha ni uongo na kuchukua vile vinavyoonyesha ni ukweli.
Ni mpaka baadaye unapokuja kugundua umedanganywa ndiyo unaona viashiria vilivyokuwepo tangu mwanzo.
Hatua ya kuchukua;
Kwa kila maamuzi unayofanya, usijipe uhakika wa asilimia 100 ya usahihi wa kile ulichoamua. Tambua akili yako inaweza kuwa imechagua kuona kile unachotaka kuona. Hivyo kabla hujafikia maamuzi yoyote, jiulize vipi kama kinyume cha ulichochagua ni kweli? Tafuta ushahidi wa kukuonyesha kwamba maamuzi uliyofanya umekosea, kisha angalia upande upi wenye nguvu kwa kuwa na ushahidi mwingi, upande kwamba upo sahihi au umekosea?
Kwa kufanya zoezi hili utaepuka kujidanganya kwenye maamuzi unayofanya.
Tafakari;
Ukweli ni mgumu kuujua na kuufikia kwa sababu mara nyingi unaona kile unachotaka kuona na kusikia unachotaka kusikia. Kuujua ukweli, jilazimishe kuona pande mbili za jambo kabla ya kufanya maamuzi.
Kocha.