2478; Njia za mkato kwenye teknolojia.
Njia za mkato kwenye safari ya mafanikio ni mtego, usizipite, maana zitakupoteza zaidi.
Lakini kwenye teknolojia, njia za mkato ni njia ya kuokoa muda na nguvu, ili uweze kutumia kwa mambo mengine muhimu.
Jana nilienda kwenye steshenari kuchapa nyaraka fulani. Kulihitajika marekebisho kabla ya kuchapa.
Mhusika akawa anafanya taratibu sana, huku mimi nikawa na haraka.
Nikamwomba nifanye marekebisho hayo haraka, akakubali. Ndani ya muda mfupi nikawa nimemaliza kufanya marekebisho hayo.
Akaniuliza umewezaje kuchagua maneno yote kwa haraka hivyo?
Nilishtushwa kidogo na swali hilo, maana niliamini kwa kuwa hizo ni kazi anazofanya kila siku, basi atakuwa anajua njia nyingi za mkato katika kurahisisha kazi yake.
Nilichukua nafasi na kumwelekeza baadhi ya njia za mkato zitakazorahisisha kazi yake.
Baada ya kumweleza nikajiuliza kama huyu hajui, huenda kuna wengine pia hawajui.
Hivyo leo nimeona ni vyema nishirikishe njia za mkato unazoweza kutumia kwenye teknolojia ili kurahisisha majukumu yako mbalimbali.
Njia za mkato ambazo nimekuwa natumia kwenye kompyuta.
1. Kuchagua maneno yote (select all) – CTR + A.
2. Kunakili maneno (copy) – CTR + C.
3. Kuweka maneno uliyokopi (paste) – CTR + V.
4. Kurudi nyuma kwenye mabadiliko uliyofanya (undo) – CTR + Z.
5. Kurudisha mabadiliko uliyofanya (redo) – CTR + Y.
6. Kuhifadhi (save) – CTR + S au F12.
7. Kubadili jina la faili (rename) – F2.
8. Kurefresh – F5
9. Kufuta moja kwa moja (permanent delete) – CTR + Delete.
10. Kuzima na kuwasha kompyuta (restat) – CTR + Alt + Delete.
Hizo ni ambazo nimekuwa natumia mara kwa mara kwenye kazi zangu za uandishi.
Kuna njia nyingine nyingi za mkato kulingana na kile ambacho kinafanyika.
Hatua ya kuchukua;
Ni kazi gani umekuwa unafanya kwa kujirudia rudia kwa kutumia vifaa vya kiteknolojia?
Hakikisha unajua njia zote za mkato kwenye kazi hiyo ili uokoe muda na nguvu katika kuifanya.
Njia za mkato kwenye teknolojia zipo, ni wewe kuzijua na kuzitumia.
Tafakari;
Ni masaa mangapi umekuwa unapoteza kila siku kwa kufanya vitu ambavyo kuna njia za mkato za kukifanya kwa haraka zaidi?
Kila teknolojia unayotumia, jua njia zake za mkato na uweze kuzifanyia kazi.
Kocha.