2479; Kufanya na kuonyesha unafanya.

Kadiri ninavyoendelea kutafakari maisha ya mafanikio, nazidi kuona jinsi nguvu ilivyo rasilimali muhimu.

Msisitizo mkubwa sana umekua unawekwa kwenye muda, kwamba una uhaba na kama mtu atashindwa kuudhibiti vizuri basi hawezi kufanya makubwa.

Lakini nguvu ndiyo rasilimali ambayo tunapaswa kuwa na udhibiti nayo mkubwa. Kwa sababu unaweza kudhibiti muda utakavyo, lakini kama utatawanya nguvu zako, hakuna makubwa unaweza kufanya.

Kila kitu unachofanya kwenye maisha yako, kinahitaji nguvu. Na nguvu unayotumia kufanya kitu kimoja, huwezi kuitumia kwenye kufanya kitu kingine.

Kufanya kazi au biashara yako kwa viwango vya juu ili ufanikiwe unahitaji kuweka nguvu.
Kuhakikisha unaonekana kweli unafanya kazi hiyo ili upate sifa kutoka kwa wengine pia inahitaji uweke nguvu.

Kitu ambacho wengi hawajui, hasa kwenye zama hizi za mitandao ya kijamii ni kwamba nguvu unazoweka kuonyesha unafanya kazi ni nguvu ambazo huwezi kuziweka kwenye kazi husika.

Chukua mfano unaweka picha za kazi zako kwenye mitandao ya kijamii. Watu wanakusifia na wengine kukuuliza maswali mbalimbali.
Inabidi utumie nguvu kufuatilia hayo, kujibu na kadhalika.
Hizo ni nguvu ambazo huwezi kuzitumia kwenye kufanya kazi yako.

Unaweza kusema lakini nafanya hivyo ili kupata wateja. Kama kweli unapata wateja kwa njia hiyo basi ni sawa.
Lakini kwa wengi, hakuna wateja wanaowapata, zaidi ya kufurahia vile wengine wanaona kazi zao na kuwaona ni muhimu.

Wateja wazuri kabisa kwa chochote unachofanya ni wale ulionao sasa. Hao ukiwapa huduma bora kabisa ambayo hawajawahi kuipata popote, watakuwa tayari kukuletea wateja wengine wazuri kama wao.

Kuwa makini sana na mtawanyo wako wa nguvu, kati ya kufanya na kuonyesha unafanya.
La sivyo utajenga sifa kubwa kwa kuwa umeweka nguvu kubwa kwenye maonyesho, ila inapokuja kwenye kazi unayofanya, inakuwa kawaida tu, kitu kinachokuzuia usipige hatua kubwa.

Haimaanishi upeleke nguvu zako zote kwenye kazi tu na kusahau mengine. Ni muhimu pia watu waendelee kujua upo na unafanya nini. Lakini tengeneza sifa yako kwa matokeo ya kazi zako na siyo kwa matokeo ya maonyesho zaidi.

Hatua za kuchukua;
Jitathmini kwenye kazi au biashara unayofanya na ona ni kiasi gani cha nguvu unachoweka kwenye kufanya na kiasi unachoweka kwenye kujionyesha kwa wengine unafanya.
Chagua kuweka nguvu kubwa kwenye kufanya na siyo kwenye maonyesho.

Tafakari;
Kutunza nguvu zako kwa yale muhimu ndiyo siri kubwa kabisa ya mafanikio. Usikimbie pale unapoweza kutembea, usisimame pale unapoweza kukaa. Kwa kila matumizi ya nguvu unayotaka kufanya, hakikisha unayaweka sehemu sahihi.

Kocha.