2480; Ishi ulaumiwe, kufa usifiwe.
Nikiwa kwenye basi safarini niliona igizo moja la kichekesho, lakini pia lenye funzo kubwa.
Palikuwa na bwana mmoja ambaye alikuwa na uwezo mkubwa kwenye mtaa wake kuwazidi wengine.
Kila mtu kwenye mtaa wake alipopata shida alienda kumwomba msaada.
Na yeye hakuwa mtu wa kukataa, pale mtu alipokuja kwake kuomba msaada, alimsaidia kwa moyo mmoja.
Hilo lilifanya baadhi ya watu kuanza kumshuku na kusema huenda ni mshirikina, hivyo anapowasaidia watu anachukua nyota zao.
Baadaye akaja kupata matatizo ya figo ambayo yalimsumbua sana. Uwezo wake wote ukaisha na mali alizokuwa nazo zikapotea.
Katika wengi aliowasaidia, ni mmoja pekee aliyekuwa tayari kumsaidia.
Wengine hata walipoombwa kuchagia fedha za matibabu, walikataa.
Baada ya muda bwana huyo akafariki dunia na hapo kila mtu kwenye mtaa akaonekana kuwa na simanzi na kusifia jinsi bwana huyo alikuwa msaada kwao.
Ni ujumbe mfupi ambao upo kwenye igizo hili, lakini una maana kubwa sana, hasa kwenye safari ya mafanikio.
Unapokuwa hai, tegemea kupata lawama. Haijalishi umefanya vitu vizuri kiasi gani, jua kuna watu ambao watachagua kukulaumu kwa kile unachofanya.
Hili ni muhimu sana kujua na kuzingatia kwenye safari yako ya mafanikio, ili uchague kufanya yale yenye maana kwako na siyo kutaka kumridhisha kila mtu, kwa sababu hilo haliwezekani.
Utakapokufa, kuna wengi watakusifia, wengi ambao hawakukuambia chochote wakati ukiwa hai.
Na hili ndiyo siyo la kujali kabisa maana ukishakufa, hutasikia tena hizo sifa zao.
Hivyo wewe fanya kile kilicho sahihi, kwa sababu ni kitu sahihi kufanya.
Usifanye kwa sababu unataka kumridhisha kila mtu, hilo halitakuja kutokea, wapo watakaokulaumu tu.
Na pia usifanye kwa sababu unataka kusifiwa, sifa nyingi unazostahili hazitatolewa mpaka utakapokufa.
Hatua ya kuchukua;
Panga kufanya mambo kwa kuangalia usahihi wake na mchango wake kukufikisha kwenye mafanikio unayoyataka.
Epuka kufanya mambo kutaka kumridhisha kila mtu au kupewa sifa na wengine.
Tafakari;
Waswahili wanaposema ubinadamu kazi, wanamaanisha kazi kweli kweli na lazima ujiandae nayo la sivyo maisha yatakuwa magumu zaidi kwako.
Kocha.