2481; Nitafanya wakati mwingine.
Hapana, hutafanya.
Ila hutaki kujiumiza kwa kujiambia kwamba hutafanya.
Hivyo unachagua kujidanganya ili ujisikie vizuri.
Lakini kujisikia vizuri bila ya kupata unachotaka haina tofauti na kutumia kilevi.
Unapata raha kwa muda, ila hakuna kinachobadilika kwenye maisha yako.
Kuyabadili maisha yako, lazima uchague kufanya kitu, siyo kutaka kufanya na wala siyo kupanga kufanya, bali kufanya.
Lakini kufanya siyo rahisi, unadhani kwa nini wengi hawafanyi?
Ni kugumu kwa kuanzia ndani yako mwenyewe.
Halafu kuna ugumu wa nje, unaotokana na changamoto na vikwazo mbalimbali.
Hivyo haitakuwa rahisi na kama hujajitoa kweli, utapata kila sababu na kisingizio kwa nini usifanye sasa na ufanye baadaye.
Ukishasikiliza sababu hizo tu na kukubaliana nazo, jua umekwisha kabisa.
Kama umepanga kufanya, fanya. Na siyo usubiri mpaka ujisikie kufanya au mpaka kila kitu kiwe tayari.
Kujiambia utafanya wakati mwingine, ni kujidanganya tu, kwani ukweli ni hutafanya.
Hatua ya kuchukua;
Jikumbushe ni mambo mangapi huko nyuma umewahi kujiambia utafanya baadaye na hukuyafanya kabisa?
Kuanzia sasa, kila unapojiambia utafanya baadaye, jikamate na ujiambie ukweli kabisa kwamba hutaki kufanya.
Halafu anzia hapo kujihoji, kwa nini hutaki kufanya?
Utakuwa mkweli kwako na utapata suluhisho la kufanya kama ulivyopanga au kutokufanya kabisa.
Tafakari;
Unapojiambia utafanya wakati mwingine, nani amekuhakikishia utapata huo wakati mwingine?
Na hata ikitokea umeupata, umejuaje kama sababu unazojipa sasa hazitakuwepo?
Kama unataka kufanya fanya, kama hutaki jiambie ukweli na siyo kujidanganya kwa kutumia baadaye.
Kocha.