2482; Madeni.

Wengi wakisikia madeni huwa wanawaza fedha.
Pale wanapokuwa wanadaiwa fedha na watu au taasisi fulani.

Lakini madeni ni dhana pana.
Chochote ambacho ulipaswa kufanya kwa wakati fulani na hukufanya, kinakuwa deni.
Na deni lolote ni kikwazo kwenye safari ya mafanikio.

Kama hupati muda wa kutosha wa kulala, unakuwa na deni la usingizi.
Deni hilo litagharimu sana umakini na ufanisi wako kama hutalilipa.

Kama hujifunzi na kwenda na mabadiliko yanayotokea unakuwa na deni la kielimu.
Deni hilo litapelekea ushindwe kutumia fursa mbalimbali zinazojitokeza.

Kama hutumii teknolojia mpya zinazokuja katika kurahisisha kazi zako unakuwa na deni la kiteknolojia.
Deni hilo litasababisha uwe na ufanisi wa chini na kutumia gharama kubwa.

Kama huweki umakini wa kutosha kwenye afya yako unatengeneza deni la afya.
Deni hilo litapelekea upatwe magonjwa mbalimbali yatakayokuwa kikwazo kwa mapambano yako.

Madeni ni mengi, umeshajionea mwenyewe ni kwa namna gani tunayatengeneza na yakawa kikwazo.

Hatua ya kuchukua;
Ni madeni gani umeyatengeneza kwenye maisha yako ambayo yanakuwa kikwazo kwako kupiga hatua na kupata mafanikio?
Orodhesha madeni yote uliyonayo kwenye maisha yako, yale yote ambayo ulipaswa kufanya ila hukuyafanya kwa wakati.
Na unajua dawa ya deni ni nini, kulipa. Hivyo lipa madeni yote uliyolimbikiza mpaka sasa.

Tafakari;
Usipolipa deni, halisimami, bali riba yake inaendelea kukua. Jua madeni yako na uyalipe mapema ili yasiwe kikwazo kwako kufanikiwa.

Kocha.