2489; Muda na thamani.
Zamani watu walikuwa wakipima kazi kwa muda ambao wamefanya.
Aliyefanya kazi kwa muda mrefu alikuwa amefanya zaidi kwa sababu kazi zilikuwa za kutumia nguvu zaidi kuliko akili.
Lakini kwa sasa mambo yamebadilika, kazi nyingi ni za kutumia akili zaidi kuliko nguvu.
Na kwa kazi hizo za akili, muda siyo kipimo sahihi cha kazi iliyofanyika. Thamani iliyozalishwa ndiyo kipimo sahihi.
Watu hawajali umefanya kazi kwa muda gani, bali wanajali umezalisha thamani kubwa kiasi gani.
Kazi za akili zinategemea sana maamuzi ambayo mtu unafanya. Na maamuzi bora huwa yanafanyika mtu akiwa na utulivu na mapumziko ya kutosha.
Hivyo kwa kazi za akili, kufanya masaa mengi ni kupunguza ubora wa kazo, maana utaanza kufanya makosa kwenye maamuzi na kuathiri kazi.
Badili namna unapima kazi unazofanya, badala ya kupima kwa muda, pima kwa thamani unayozalisha.
Unapozalisha thamani kubwa, watu watakuwa tayari kukulipa zaidi bila kujali umefanya kazi kwa muda gani.
Ukijiwekea ukomo kwenye muda wa kufanya kazi, unautumia muda vizuri na kuacha kuupoteza.
Unapokosa ukomo kwenye muda wa kazi, kwa kuona una muda mwingi, unaupoteza kwenye mambo mengi yasiyohusu kazi.
Ukiwaangalia wale wanaosema wanafanya kazi masaa mengi, kuna muda mwingi wanaupoteza ambao hawafanyi kazi husika.
Kufanya kazi huku unaruhusu usumbufu wa simu au kuingia mitandaoni inaathiri sana ubora wa kazi. Hata kama utafanya muda mrefu kiasi gani, kazi hiyo haiwezi kuwa bora.
Jipime kwa thamani unayozalisha na siyo kwa muda unaofanya kazi. Watu wanakuja kwako kwa namna wanavyoweza kunufaika wao. Muda wako wa kazi hauwezi kuwanufaisha, ila thamani unayozalisha inawanufaisha.
Hatua ya kuchukua;
Umekuwa unapimaje ufanyaji wako wa kazi au biashara yako? Kama majukumu yako ni ya kutumia nguvu kuliko akili, muda una nafasi kubwa. Lakini kama majukumu yako yanatumia akili kuliko nguvu, thamani unayozalisha ina nafasi kubwa.
Kwa vyovyote vile, jipime kwa thamani unayozalisha na unapopanga kufanya kazi, iwe ni kazi tu, usiruhusu usumbufu mwingine kuingilia kazi unayofanya.
Ubora wa kazi unategemea sana utulivu na umakini wako kwenye kile unachofanya.
Tafakari;
Wanaolipwa mara kumi ya wengine haimaanishi kwamba wanafanya kazi mara kumi ya wanavyofanya wengine. Badala yake wanazalisha thamani mara kumi ya wanavyozalisha wengine. Kabla hujakimbilia kufanya kazi zaidi, angalia ni thamani ipi ukiongeza utalipwa zaidi na fanya hivyo.
Kocha.