2493; Unapoteza Ulichonacho.

Changamoto nyingi kubwa kwenye maisha majibu yake huwa ni rahisi kabisa.

Lakini tumekuwa hatukubali wala kufanyia kazi majibu hayo kwa sababu ya urahisi wake, tunaona hayawezi kuwa sahihi.

Ni majibu hayo rahisi tunayoyapuuza kwenye maisha ndiyo yamekuwa kikwazo kikubwa kwetu kupiga hatua kubwa.

Leo tuangalie mfano wa kupoteza.
Kila mtu ni mhanga wa hili, umekuwa unapoteza vitu mbalimbali.
Lakini vikubwa kabisa ambavyo tumekuwa tunapoteza na kuwa kikwazo kwenye mafanikio ni fedha, muda na nguvu.

Ni mara ngapi ukiwa huna fedha unakuwa na mipango mizuri kabisa, ila ukizipata mipango hiyo inayayuka?

Najua umekuwa unashangazwa na hili, ukiwa bize unafanya mengi na makubwa kuliko ukiwa na muda mwingi.

Yote hayo yanatokana na kitu kimoja kikubwa, unapoteza ulichonacho.

Kwa kifupi ni kama unapoteza kitu ni kwa sababu unacho kwa wingi.
Hivyo kama unataka udhibiti upotevu wa kitu, anza kwa kupunguza kuwa na wingi wa vile ambavyo umekuwa unapoteza sana.

Kama tatizo lako limekuwa ni upotevu wa muda, anza kuhakikisha muda wako wote umepangilia kwa mambo muhimu ili usiwe na muda ambao huna cha kufanya na ukaishia kuupoteza.

Kama tatizo lako ni upotevu wa fedha, hakikisha unadhibiti fedha zako kiasi kwamba unakuwa huna fedha ambayo haina mipangilio na hivyo huwezi kupoteza.

Na hata kwenye nguvu, kama unajikuta unapoteza nguvu zako kwenye mambo yasiyo na tija, ni kwa sababu zinakosa matumizi ya tija. Pangilia nguvu hizo kwenye matumizi ya tija na yanayokuchosha na hutazipoteza hovyo.

Kama huna cha kupoteza, huwezi kupoteza. Hivyo kupunguza upotevu kwenye maisha yako, dhibiti kiasi unachokuwa nacho kwenye kile unachopoteza.

Hatua ya kuchukua;
Angalia kile ambacho umekuwa unapoteza sana kwenye maisha yako na kuwa kikwazo kwako. Kisha punguza kiasi unachokuwa nacho ili kusiwe na upotevu.
Jidhibiti sana kiasi kwamba unakuwa huna cha kupoteza.
Usiwe na kitu chochote ambacho hakina mipango au matumizi ya uhakika.

Tafakari;
Huwezi kupoteza kitu ambacho huna, hivyo hatua ya kwanza ya kudhibiti upotevu ni kuhakikisha huna cha kupoteza.

Kocha.