2496; Unachokosa siyo unachodhani.
Ni rahisi kuona hujapiga hatua kwenye maisha kwa sababu kuna vitu umekosa.
Lakini kwa sehemu kubwa unachokosa siyo kile unachodhani.
Unachodhani unakosa ni kikubwa na kilicho nje ya uwezo wako.
Lakini unachokosa kwa uhalisia ni kidogo na kipo ndani ya uwezo wako.
Hujakosa kipaji, bali unachokosa ni subira na uvumilivu.
Unaweza kusingizia kukosa kipaji kama sababu ya kukwama. Lakini siyo kweli, subira na uvumilivu vinashinda kipaji kila mara. Hata kama huna kipaji kabisa, ukichagua kufanya kitu na ukakifanya bila kuacha, lazima utafanikiwa.
Hujakosa mawazo, unachokosa ni kuchukua hatua.
Ni rahisi sana kujiambia kwamba hujapata wazo zuri la kufanya kitu. Mawazo ni mengi sana na yanapatikana kirahisi, ni kuchukua hatua ndiyo kikwazo kwako.
Hujakosa fursa, bali unakosa ujasiri wa kuchukua hatua ambazo hujazoea.
Unapenda sana mazoea na vitu vipya unaviona siyo sahihi. Fursa zipo kwenye vitu vipya ambavyo hujazoea kuvifanya. Ukianza kukabili vitu vipya, fursa zitakuwa nyingi kwako.
Hatua ya kuchukua;
Tafakari ni vitu gani umekuwa unajiambia unakosa na kupelekea ushindwe kupiga hatua. Kisha chimba ndani na uone kama kweli ndiyo unachokosa au ni kisingizio tu.
Kwa sehemu kubwa, unachokosa siyo unachodhani.
Na kuthibitisha hilo, angalia kama hakuna wengine wameweza licha ya kukosa kile unachosema umekosa.
Tafakari;
Ni rahisi kujifariji na visingizio kuliko kuchukua hatua. Lakini visingizio haviwezi kukupa kile unachotaka. Hivyo chagua visingizio au chagua kupata unachotaka. Huwezi kuwa na vyote viwili vya pamoja.
Kocha.