#SheriaYaLeo (3/366); Sauti Ya Ndani.
Watoto wadogo huwa wanajua kwa hakika nini wanapenda na nini hawapendi.
Huwa hawaigizi maisha na hawafanyi chochote kuwaridhisha wengine.
Kama kitu wanakipenda wanafanya, kama hawakipendi hawafanyi.
Watoto hao wanaongozwa na sauti kuu iliyo ndani yao, sauti inayotokana na ule uwezo ambao upo ndani yao.
Hawafanyi kitu kutokana na wengine, bali wanafanya kitu kutokana na wao wenyewe.
Lakini kadiri mtu anavyokua, jamii inaanza kumjaza sauti nyingine za nini anapaswa kufanya na nini hapaswi kufanya.
Jamii inamlaghai akifanya nini ndiyo atakuwa mtu mzuri na akifanya nini atakuwa mtu mbaya.
Hilo linamfanya mtu aanze kuishi maisha ya kuigiza na kudanganya ili tu kuwaridhisha wengine.
Matokeo yake ni mtu kuisahau sauti ya ndani na kuhangaika na sauti za dunia.
Mtu kufanya mambo mengi yasiyokuwa na tija kabisa.
Na hilo ndiyo limefanya wengi kuwa na maisha ya kawaida, maisha yasiyo na mafanikio makubwa.
Unataka kushika hatamu ya maisha yako, hatua muhimu ni kurudi kwenye sauti yako ya ndani.
Sauti ambayo inakujua vizuri na sauti ambayo haijawahi kuzimishwa na kitu chochote.
Isikilize sauti hiyo na iruhusu ikuongoze kwenye vitu gani ufanye.
Hapo utaweza kufanya vitu ambavyo vinatoka ndani yako kweli na ukavifanya kwa viwango vya juu kabisa.
Sheria ya leo; Leo fanya kitu kimoja ambacho ulipenda sana kufanya ulipokuwa mtoto. Isikilize sauti iliyo ndani yako na iruhusu ikuongoze.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma