Rafiki yangu mpendwa,
Maisha huwa hayaendi vile tunavyotaka sisi mara zote.
Huwa yana vikwazo na changamoto mbalimbali.
Unaweza kuweka mipango yako vizuri, unaweza kuchukua kila hatua unayopaswa kuchukua, lakini matokeo unayokuja kupata ni tofauti kabisa na ulivyotegemea kupata.
Hivyo ndivyo maisha yalivyo, hivyo ndivyo asili inavyofanya mambo yake na wewe siyo mtu wa kwanza mambo ya aina hiyo kutokea kwako.
Kwa kuwa wengi tunaingia kwenye maisha bila ya maandalizi kamili, kwa kuwa tunategemea kupata kila tunachotaka, huwa hatupo tayari kukabiliana na hali kama hiyo ya kukosa unachotaka.
Hivyo hali hiyo inapotokea, tunakimbilia kuikwepa, kuisahau au kujaribu kuachana nayo.
Hivyo tumekuwa tunatafuta usumbufu mbalimbali wa kuondoa akili zetu kwenye hali ambayo hatuitaki.

Usumbufu rahisi umekuwa ni chupa (pombe na vilevi vingine). Wengi wanapokutana na magumu kwenye maisha, wamekuwa wanakimbilia vilevi mbalimbali kama sehemu ya kusahau magumu hayo.
Kinachotokea ni magumu yanaendelea kuwa makubwa na kuwa kikwazo zaidi.
Usumbufu mwingine rahisi zaidi kwenye zama za sasa ni mitandao ya kijamii.
Ni rahisi sana kukimbilia kwenye mitandao hiyo pale mambo yanapokuwa magumu, kwa sababu huwa inatoa raha za haraka na za muda mfupi.
Pia wengi wamekuwa wanatumia mitandao hiyo kama sehemu ya kupata faraja pale mambo yanapokuwa magumu.
Wanayaweka mitandaoni na kutegemea kupata faraja kwa wengine.
Kukimbilia kusoma vitu vinavyohamasisha na kuleta matumaini ni usumbufu mwingine ambao watu huukimbilia wanapokuwa na matatizo mbalimbali. Hakuna ubaya wowote kusoma vitu chanya na vya kutia moyo, lakini kama unavisoma tu hivyo huku ukiliacha tatizo bila kulikabili, huo ni usumbufu na hautakusaidia kwa namna yoyote ile.
Kuna njia nyingine ambazo watu wamekuwa wanatumia kutoroka matatizo yao, ngono pia ipo, kufuatilia zaidi mambo ya wengine ipo, kutengeneza msongo kiakili pia ipo.
Rafiki yangu, leo nina ujumbe mfupi sana kwako kuhusu kuyajenga maisha yako kwa usahihi. Hakuna tatizo limewahi kutatuliwa kwa kukimbiwa. Hakuna kiwango chochote kile cha usumbufu au kulificha tatizo kutalifanya liondoke au kupata suluhisho.
Njia zozote unazokimbilia wakati wa tatizo ni kujidanganya tu.
Tatizo huwa linatatuliwa kwa kukabiliana nalo. Kwa kukubali kuna tatizo, kujua chanzo cha tatizo, kuangalia njia za kulitatua tatizo hilo na kisha kuhakikisha halijirudii tena.
Hiyo ndiyo namna sahihi ya kukabiliana na tatizo lolote kwenye maisha yako ili uweze kufika kule unakotaka kufika.
Kwa kila unachofanya, jua kabisa kuna nafasi ya kupata matokeo ambayo hujategemea kufanya. Hivyo kuwa na maandalizi kabisa kwamba itakapotokea umepata matokso ambayo hukutegemea, ni hatua zipi utakazokwenda kuchukua?
Na haijalishi tatizo ni kubwa kiasi gani, kuna hatua ambazo unaweza kuzichukua na kuanza kulitatua.
Hivyo kamwe usikubali kukimbia tatizo linalokukabili kwenye maisha yako.
Kufanya hivyo ni kuzidi kulipa tatizo lako nafasi ya kuwa kubwa zaidi.
Likabili kila tatizo pale unapoligundua, litatue na hakikisha unajua njia za kuzuia lisitokee tena au hata likitokea lisiwe na madhara makubwa.
Matatizo ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku. Vile unaona wengine wanapitia matatizo mbalimbali, jua na wewe pia unaweza kuyapitia. Hivyo usiyaendeshe maisha yako kama mtoto, kwa kutegemea kila wakati utapata kila unachotaka.
Jua kuna wakati mambo yatakwenda tofauti na badala ya kukimbia yanapotokea hayo, yakabili na uweze kusonga mbele.
Kadiri unavyotatua matatizo yanayokukabili, ndivyo unavyozidi kuwa imara zaidi na kuweza kuyakabili mengine zaidi.
Uzuri ni kwamba ndani yako una uwezo wa kukabiliana na tatizo lolote lile linalokukabili kwenye maisha yako. Hata kama unaliona ni kubwa na gumu kiasi gani, lisingeweza kuja kwako kama hukuwa na uwezo wa kulikabili.
Kuijua nguvu hiyo na jinsi ya kuitumia, soma kitabu cha UNA NGUVU YA KUTENDA MIUJIZA. Kitabu hicho kitakuonyesha namna sahihi ya kutumia mwili wako na akili yako kukabiliana na chochote kwenye maisha yako.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani
www.somavitabu.co.tz