2500; Wewe Ndiye Mfano.

Kama kuna watu wako chini yako na wanafanya vitu ambavyo huridhiki navyo, kuna mtu mmoja tu wa kumlaumu, wewe mwenyewe.

Ni rahisi kuwaona watu wanakuwa mzigo na kukukwamisha.
Lakini ukweli ni wao wanaiga mfano wako.

Wale walio chini yako, wanaangalia zaidi kile unachofanya kuliko unachosema.
Wataiga kwa haraka unachofanya kuliko kutekeleza unachosema.

Hivyo kama wale walio chini yako hawafanyi vile unavyotaka, kabla hujawalaumu anza kujiuliza wewe kama unafanya kile unachotaka wao wafanye.

Kama watu hawaweki umakini kwenye kazi zao, je wewe unaweka umakini kwenye kazi yako?
Kama watu hawaendi kwa kasi unayotaka, je wewe unaendana kwa kasi hiyo?
Kama watu hawawahi au kukamilisha mambo kwa wakati, je wewe unafanya hivyo?

Ni rahisi kulaumu wengine, lakini unapokuwa kiongozi, lawama zote zinaishia kwako.
Chochote kile unachotaka wengine wafanye, anza kukifanya wewe mwenyewe.
Na pale watu wanapoona unafanya kweli, wataamua nao kufanya au itawabidi wakukimbie.

Hatua za kuchukua leo;
Angalia ni kitu gani umekuwa unapenda sana wale walio chini yako wakifanye. Halafu anza kukifanya wewe mwenyewe bila hata ya kupiga kelele sana. Fanya kwa msimamo bila kuacha na utashangaa mwenyewe jinsi wengine nao watakavyoanza kufanya.

Tafakari;
Matendo yako yanapiga kelele sana kiasi kwamba watu hawawezi kusikia kile unachosema. Usijisumbue sana na kusema watu wanapaswa kufanya nini au kuwaje, bali fanya. Unapofanya watu wanaelewa zaidi na wao kulazimika kufanya pia.

Kocha.