2505; Siyo Pata Potea.

Kikwazo kikubwa cha watu kwenye mafanikio ni mtazamo wanaokuwa nao.
Ndiyo maana unaweza kukuta watu wawili, wanafanya kazi au biashara ya aina moja, mmoja anafanikiwa sana na mwingine anashindwa.
Kinachowatofautisha watu hao ni mtazamo.

Kuna mitazamo mingi ambayo imekuwa kikwazo kwa wengi kufanikiwa.
Lakini mmoja mkubwa ambao umeathiri wengi ni mtazamo wa pata potea.
Huu ni ule mtazamo wa mtu kutaka kupata unachotaka, bila kujali wengine wanapata nini.
Mtu anakuwa tayari hata kuwaumiza na kuwadhuru wengine ili tu apate anachotaka.

Huu ni mtazamo mbovu sana, wenye manufaa ya muda mfupi lakini wenye madhara ya muda mrefu.
Kwa sababu mwanzo utapata unachotaka, lakini utaharibu kabisa mahusiano yako na wengine kiasi kwamba huwezi kupata tena kitu kutoka kwao.

Kwa chochote unachofanya, angalia ni kwa namna gani mwingine ananufaika pia, ili kujenga mahusiano mazuri yatakayokuwezesha kuendelea kupata zaidi na zaidi.

Chochote unachouza, hakikisha kina manufaa kwa yule unayemuuzia, ili aendelee kununua kwako zaidi na zaidi.
Haina maana kumlaghai mtu anunue kitu ili wewe uuze lakini kisiwe na manufaa kwake, hatarudi tena kununua kwako na atasema mabaya kuhusu wewe ambayo yatakuathiri sana.

Chochote unachonunua, nunua kwa namna ambayo muuzaji atanufaika pia, ili aweze kuendelea kuuza kitu hicho na uendelee kukipata.
Haina maana kumlaghai mtu akuuzie kitu kwa namna ambayo yeye hanufaiki, akipata hasara na kushindwa kuendelea kuuza, hilo litakuathiri wewe na wengine pia.

Hatua ya kuchukua;
Katika kila unachofanya, swali la kwanza kujiuliza ni kwa namna gani wengine unaojihusisha nao wananufaika pia. Hakikisha kuna manufaa kwa wengine kabla hujafanya. Usiwe mtu wa kuangalia leo tu, angalia na kesho pia.

Tafakari;
Tamaa yoyote ya muda mfupi huwa inaishia kuwa kikwazo kwa muda mrefu. Mara zote angalia muda mrefu wa jambo kabla ya kufanya maamuzi.

Kocha.