#SheriaYaLeo (9/366); Pata hamasa kutoka kwa mashujaa wako.
Kuna watu ambao ukiwaona wanavyofanya kazi zao unapata hamasa kubwa sana ndani yako.
Unavutiwa sana na aina ya maisha wanayoishi na yale wanayofanya.
Watu hao wanakupa hamasa na msukumo wa kufanya makubwa kama wao wanavyofanya.
Hao ndiyo mashujaa wako, ambao ukiwatumia vizuri utaweza kujua kile kweli kilicho ndani yako na kuweza kufanya makubwa.
Wajue kabisa mashujaa wako ni wakina nani kisha watumie kama mwongozo kwenye maisha yako.
Kwanza kabisa tumia msukumo mkubwa wanaokupa kujisukuma kufanya makubwa kama wao. Kwa kuwa kuna moto wanawasha ndani yako, endelea kuuchochea huo moto.
Pili watumie kama njia ya wewe kujipima, kuona ni kwa viwango gani unafanya. Unapofanya mwenyewe ni rahisi kuona umefanya makubwa. Lakini unapojipima kwa kuwatumia mashujaa wako, unaona bado hujafanya makubwa kama wao.
Tatu watumie kama njia ya kufanya maamuzi hasa unapokuwa njia panda. Pale ambapo huna uhakika nini ufanye, jiulize angekuwa shujaa wako angefanya nini. Hilo litakusaidia kufanya maamuzi sahihi.
Sheria ya leo; Je kuna watu ambao kazi zao zinakupa hamasa na msukumo mkubwa ndani yako? Watambue watu hao na watumie kama mfano na mwongozo kwako.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma