2506; Kitakachokutoa Njia Panda.
Mara kwa mara huwa tunajikuta kwenye njia panda fulani katika safari yetu ya maisha.
Kutokana na mambo mbalimbali yanayokuwa yanaendelea, unakuwa hujui nini hasa ufanye kati ya mengi yaliyo mbele yako.
Ni katika hali hizi za njia panda ndipo wanaofanikiwa na wanaoshindwa hutofautiana.
Wanaofanikiwa huwa wana kanuni ya kuondoka kwenye kila njia panda wanayokuwa wamejikuta.
Wanaoshindwa huwa wanaganda kwenye njia panda zao na kushindwa kupiga hatua.
Hapa kuna kanuni rahisi ya kukutoa kwenye njia panda yoyote ile.
Unapojikuta kwenye njia panda, tumia kanuni hii kutoka hapo. Kanuni ina vitu vitatu.
Kitu cha kwanza ni weka kazi zaidi.
Angalia ni fursa gani zilizopo za kuweka kazi zaidi na zifanyie kazi.
Haijalishi upo kwenye njia panda gani, angalia kazi gani unaweza kufanya na uifanye.
Kitu cha pili ni uaminifu.
Unapokuwa njia panda, kuwa mwaminifu, sema ukweli na fanya kilicho sahihi.
Wengi wanapojikuta njia panda hujipoteza zaidi kwa kukosa uaminifu.
Kitu cha tatu ni kuwasaidia wengine.
Wengi hukwama kwenye njia panda kwa sababu wanajiangalia zaidi wao wenyewe.
Huwezi kutoka kwenye mkwamo kwa kujiangalia mwenyewe, maana utazidi kukwama.
Unatoka kwenye mkwamo kwa kuangalia watu gani unaweza kuwasaidia.
Hata uwe unapitia nini, kuna watu unaweza kuwasaidia.
Angalia watu hao na chukua hatua ya kuwasaidia, utashangaa jinsi itakavyokuwa rahisi kutoka kwenye mkwamo wako.
Hatua ya kuchukua;
Je una msingi wowote uliojijengea wa kuondoka kwenye mkwamo?
Kama huna ujenge sasa kwa haya matatu uliyojifunza hapa.
Tafakari;
Maisha ni kile kinachotokea wakati unahangaika na mambo mengine. Unapokuwa kwenye mkwamo, usihangaike sana na mkwamo huo, bali kuwa na mambo mengine unayohangaika nayo na utatoka kwenye mkwamo huo.
Kocha.