Rafiki yangu mpendwa,

Steve Jobs alikuwa na viwango vya juu mno na hakukubali hata kidogo chini ya viwango hivyo.
Aliwasukuma watu mpaka wavifikie na hakuwa na huruma kwenye viwango vyake.
Hili lilimfanya aonekane ni wa ajabu, katili na asiyejali.
Lakini aliweza kuleta mapinduzi makubwa kwenye teknolojia ambayo mpaka leo tunayafurahia.

Elon Musk huwa anafanya kazi masaa 120 kwa wiki, wakati mwingine akilala hapo hapo kwenye kazi yake. Huwa hachukui likizo kwenye kazi na huwa hajilipi mshahara wowote.
Kipaumbele chake cha kwanza ni kazi.
Amekuwa anaonekana ni wa ajabu, asiyejijali na anayeharibu maisha yake.
Lakini leo ndiyo mtu tajiri kuliko wote duniani, huku akileta mapinduzi kwenye sekta ya usafirishaji na anga.

Warren Buffett amekuwa anaishi kwenye nyumba aliyonunua miaka 60 iliyopita.
Huwa ananunua hisa za makampuni anayoyaelewa tu na akishanunua hauzi hovyo.
Watu wamekuwa wanamuona ni wa ajabu, wakimwona anakosa fursa nzuri kwa kutonunua hisa za makampuni ya teknolojia.
Lakini yeye ni mwekezaji mkubwa na ambaye amekusanya utajiri mkubwa sana.

Hendry Ford aliwaambia mainjinia wake anataka injimi ya V8. Mainjinia wakamwambia hilo haliwezekani kifizikia. Akawaambia anaitaka au kama hawawezi atawafukuza kazi. Alionekana ni mjinga anayelazimisha mambo kwa sababu hana uelewa. Lakini injini ya V8 ilipatikana na mpaka leo imekuwa na manufaa.

Wright Brothers walikuwa mafundi baiskeli ambao walikuwa na ndoto ya kuendesha chombo angani. Walifanyia kazi kila siku kwenye karakana yao. Watu waliwacheka na kusema hao vijana wamechanganyikiwa.
Wanafizikia walisema kuendesha chombo angani ni jambo ambalo haliwezekani kabisa kifizikia, labda miaka elfu moja inayo.
Ndani ya mwaka huo huo Wright Brothers wakarusha chombo chao na mpaka leo tunafaidika na usafiri wa anga.

Nelson Mandela alifungwa jela na makaburu kwa miaka 27. Alipitia mateso mengi katika kipindi hicho chote. Lakini alipotoka alisamehe yote na kuleta maridhiano. Wengi walimwona ni mtu wa ajabu, aliyekubali kulaghaiwa na makaburu. Lakini leo hii amekuwa alama ya uvumilivu na ushindi kwenye maisha.

Julius K. Nyerere alikuwa ni mwalimu kwenye serikali ya kikoloni. Alikuwa na kazi nzuri ukilinganisha na watu wengine, kitu ambacho kingeweza kumfanya aridhike na kutokuhangaika. Lakini alikuwa tayari kupoteza kazi hiyo ili kupigania uhuru wa Tanganyika. Na harakati zake zikaiwezesha Tanganyika kuwa huru.

Je wewe ni kitu gani ambacho watu wanakiona ni cha ajabu kwako?
Hapo ndipo nguvu zako za kufanya makubwa zilipo.
Usifiche huo uajabu wako, uishi wazi na utaweza kufanya makubwa sana kwenye maisha yako.

Lakini lazima ujue utakapouishi uajabu wako kuna watu utawakera sana.
Kuna watu watakukosoa, kukupinga, kukudhihaki na hata kutumia uajabu huo kukuwekea vikwazo mbalimbali.

Usitishwe wala kukwamishwa na watu hao.
Kubali na ishi uajabu wako, kwani hapo ndipo penye mafanikio yako makubwa.

Tenga muda leo na ujitafakari ni uajabu gani upo ndani yako.
Huenda umekua unauficha au kuupuuza.
Sasa ni wakati wa kuufufua na kuuishi.

Na kikubwa unachopaswa kujua ni kwamba ndani yako tayari una nguvu ya kufanya makubwa kuliko ambavyo umekuwa unafanya.
Kama bado hujaanza kutumia nguvu hiyo, pata sasa kitabu cha UNA NGUVU YA KUTENDA MIUJIZA na uweze kuijua, kuifikia na kuitumia nguvu iliyolala ndani yako sasa.

Kupata kitabu hicho wasiliana na 0752 977 170 na utatumiwa au kuletewa kitabu ulipo.
Usikubali uajabu wako upotee, usiache nguvu kubwa iendelee kulala ndani yako.
Ni wakati wa kuamka na kuwa wewe ili uweze kufanya makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.somavitabu.co.tz