2517; Kuiga mafanikio ni kujipoteza.

Pamoja na siri nyingi za mafanikio kuwa bayana.
Pamoja na hadithi za watu waliofanikiwa kupatikana kwa urahisi kila mahali.
Bado ni wachache sana wanaopata mafanikio makubwa.

Tulidhani kwenye zama hizi ambapo maarifa ya mafanikio yanapatikana kwa wingi na urahisi basi wengi wangekuwa wamefanikiwa, lakini hali ni tofauti.

Na hilo limetokana na tabia yetu binadamu kuiga. Tukiona kitu kinafanya kazi kwa wengine, tunakimbilia kukiiga kwa kudhani kitafanya kazi kwetu pia.

Ndiyo maana mtu akianzia biashara mpya mahali, haichukui muda wengine wanaiga.
Na fursa mpya inapoonekana, kila mtu anaikimbilia.

Hatupendi vitu vigumu vya kufikiria, tunapenda vitu rahisi vya kuiga.
Sasa kwenye mafanikio, kuiga ni sumu kubwa.
Hakuna aliyewahi kufanikiwa kwa kuiga.
Hata aliyefanikiwa, ikiwa ataanza tena na kurudia yale yote aliyofanya, hatapata mafanikio aliyopata.

Kila tukio kwenye safari ya mafanikio huwa linatokea mara moja tu, hivyo kurudia kitu kile kile huwezi kupata matokeo yale yale.

Hivyo kwenye mafanikio usiige yale ambayo wengine wanafanya au walifanya.
Bali iga mtazamo walionao, iga mchakato wanaotumia kufanya maamuzi na kufanya mambo yao.
Na muhimu zaidi, jifunze kwao umuhimu wa kuwa wewe na kuishi kwa uhalisia wako.
Maana hakuna aliyeweza kufanikiwa bila ya kuwa yeye halisi.

Kama kuna kitu kimoja cha kuiga kutoka kwa wale waliofanikiwa basi ni kuiga kuwa wewe halisi na siyo kuigiza maisha.

Hatua ya kuchukua;
Kila unapojifunza siri au hadithi za mafanikio ya wengine, usijiambie na mimi nitafanya kama yeye. Bali jiulize uliyojifunza yanawezaje kuendana na wewe kwa hali tofauti uliyonayo?
Boresha chochote unachojifunza kiweze kuendana na wewe ili kiwe na manufaa kwako.

Tafakari;
Kama kujua siri za mafanikio ndiyo ingekuwa kufanikiwa, kila mtu zama hizi angekuwa amefanikiwa. Lakini mafanikio siyo rahisi hivyo, mafanikio yanataka uwe wewe na siyo kuiga wengine. Na hakuna kitu kigumu hapa duniani kama kuwa wewe. Ukiliweza hili, utayaweza mafanikio makubwa.

Kocha.