#SheriaYaLeo (21/366); Kuwategemea wengine ni tatizo.

Hakuna kitu kibaya kama kuweka mategemeo yako yote kwa watu wengine.
Utegemezi unakuweka kwenye hatari ya kuathiriwa na hisia hasi kama usaliti, kukatishwa tamaa, kuvurugwa na msongo. Hisia hizi huharibu sana utulivu wa akili yako.

Kujitegemea mwenyewe ni muhimu sana kwa utulivu na mafanikio yako.
Kupunguza kuwategemea wengine, hasa wanaojiita wataalamu, unahitaji kujijengea ujuzi mwingi.
Unapaswa kuyaamini maamuzi yako mwenyewe.

Tambua kwamba huwa tuna tabia ya kukuza uwezo wa wengine kwa kuona wanaweza zaidi yetu na kudharau uwezo wetu wenyewe kwa kuona hatuwezi kama wengine.
Tunachosahau ni kwamba kila mtu anajiona hivyo na wengi wanakazana kuonekana wanajua wanachofanya, kumbe siyo.
Unapaswa kuvuka hilo kwa kujiamini wewe mwenyewe kuliko unavyowaamini wengine.

Ni muhimu kukumbuka kwamba kujitegemea haimaanishi kujipa mzigo wa vitu vidogo vidogo.
Unapaswa kuwa na uwezo wa kutofautisha mambo madogo ya kuwaachia wengine na makubwa ambayo yanahitaji umakini wako.

Sheria ya leo; Kuwategemea wengine ni kujitengenezea matatizo; kujitegemea mwenyewe ni kupata nguvu na mamlaka.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma