2518; Mabadiliko na Msimamo.

Kwenye safari ya mafanikio na maisha kwa ujumla, kuna njia panda moja kubwa ambayo wengi huwa hawaielewi.
Kuna mambo ambayo yanabadilika kila wakati.
Na kuna mambo ambayo hayabadiliki kabisa.

Njia panda inakuwa ni kujua mambo gani yanabadilika ili kubadilika nayo na mambo gani hayabadiliki ili kuwa na msimamo nayo.

Mambo yanayohusu mchakato huwa yanabadilika. Kadiri teknolojia zinavyobadilika michakato inarahisishwa zaidi.

Mambo yanayohusu tabia za watu huwa hayabadiliki. Hata teknolojia zibadilike kiasi gani, watu wanabaki kuwa watu.

Tukiangalia mfano wa biashara, michakato inabadilika kila siku, kama kuuza kwa kutumia mtandao wa intaneti na mengine. Lakini mahitaji ya watu ni yale yale, kupata kitu kinachotatua matatizo au mahitaji yao kwa bei ambayo wanaimudu.

Hivyo katika kuweka mipango yako, badilika na mambo yanayobadilika na kuwa na msimamo kwenye mambo yasiyobadilika.
Kwenye biashara, mara zote kazana kutoa thamani kubwa kabisa kwa wateja wako. Huku ukitumia teknolojia mbalimbali kutoa na kufikisha thamani hiyo kwa wateja.

Hatua ya kuchukua;
Kwenye kazi au biashara unayofanya, ainisha ni vitu gani vinavyobadilika na vitu gani ambavyo havibadiliki. Badilika na vinavyobadilika huku ukiwa na msimamo kwa yasiyobadilika.

Tafakari;
Mabadiliko ni sehemu ya maisha, yajue na uendane nayo. Msimamo ni sehemu ya tabia za binadamu, zijue na uweze kuzitumia vizuri.

Kocha.