2519; Tatizo siyo muda, bali nguvu.
Nimeshaliandikia hili hapa mara kadhaa, lakini nitaendelea kulirudia kwa sababu ni dhana ambayo wengi hawaielewi.
Tumezoeshwa sana kuhangaika na muda. Tukafundishwa jinsi ya kupangilia na kudhibiti muda wetu ili kuweza kufanya makubwa.
Tumekuwa tunaambiwa wazi kabisa kwamba muda ni zaidi ya fedha, maana ukipoteza fedha unaweza kupata nyingine, ila ukipoteza muda huwezi kuupata tena.
Hayo yana ukweli mkubwa, lakini ukweli huo hatujakamilika. Kudhibiti muda pekee hakutoshi wewe kufanya makubwa, unahitaji kupangilia na kudhibiti nguvu zako pia.
Labda twende na mfano ambao utaweza kuuelewa vizuri.
Una simu yako janja, ambapo ndani yake kuna tamthilia nzuri sana unayotaka kuiangalia.
Unatenga muda ambapo utaangalia tamthilia hiyo, baada ya kuwa umemaliza majukumu fulani.
Wakati unafanya majukumu hayo ukafungulia muziki kwenye simu hiyo na kuwa unasikiliza. Kwa kuwa una shauku ya kuangalia tamthilia uliyopanga, unapata msukumo wa kukamilisha majukumu uliyonayo kwa wakati.
Kweli unayamaliza majukumu hayo na sasa unakaa chini ili uanze kuangalia tamthilia yako. Unapoichukua simu ili uanze kuangalia tamthilia, unagundua simu haina chaji, imebaki asilimia 1 pekee na hivyo itazima muda siyo mrefu.
Unafungua tu tamthilia kuangalia, simu inazima na kwa bahati mbaya sana umeme hakuna.
Kwa hiyo hapo muda unao wa kutosha kabisa, ila simu haina chaji na hivyo muda ulionao unakosa maana.
Hivyo ndivyo sisi binadamu tulivyo, miili yetu ni kama simu, unapoianza siku unakuwa umejaa chaji. Kadiri siku inavyokwenda na ukafanya majukumu mbalimbali chaji hiyo inapungua.
Hivyo basi, unapopangilia na kudhibiti muda wako, kumbuka pia kupangilia na kudhibiti nguvu zako.
Kwa kuwa haitakuwa na maana kuwa na muda mwingi huku ukiwa umechoka kabisa, hakuna makubwa utakayoweza kufanya.
Hatua ya kuchukua;
Majukumu yote muhimu yapange kuyafanya wakati ambao una nguvu za kutosha.
Na mara zote tunza nguvu zako, usizipoteze hovyo kwa mambo yasiyo na tija.
Kama huna cha muhimu kufanya ni bora kupumzika kuliko kupoteza nguvu zako kwenye mambo ya hovyo.
Tafakari;
Mara zote tunza nguvu zako, usikimbie pale ambapo kutembea kunatosha na usisimame pale ambapo kukaa kunatosha.
Kocha.