#SheriaYaLeo (23/366); Yagawe malengo yako makubwa kwenye vipande vidogo.

Kuwa na malengo makubwa na ya muda mrefu kunakupa msukumo na umakini mkubwa wa kuyafikia.
Malengo hayo ambayo ni makubwa, mfano biashara kubwa ya kujenga huwa yanakupa shauku kubwa na kukusukuma uwe bora zaidi.

Lakini pia malengo hayo makubwa huwa yana tatizo moja, huwa yanakupa hofu na wasiwasi pale unapoyaangalia kwa ukubwa wake na pale ulipo sasa.
Kuondokana na hofu hizo, unapaswa kuyagawa malengo hayo makubwa kwenye vipande vidogo vidogo.

Malengo hayo makubwa ya miaka mingi, yagawe kwenye mwaka, mwezi, wiki na siku.
Kuwa na vipande vidogo kabisa vya malengo yako makubwa unavyovifanyia kazi kila siku na kuvikamilisha.
Kadiri unavyokamilisha vipande vidogo vya malengo, ndivyo unavyozidi kupata nguvu na hamasa ya kufikia malengo yako makubwa.

Kwa jukumu lolote kubwa unalokuwa nalo, ligawe kwenye vipande vidogo vidogo unavyoweza kuanza kufanyia kazi mara moja.
Hilo litakusaidia kuepuka kupoteza muda na nguvu zako kuhofia ukubwa wa kitu na kukikwepa kwa kuhangaika na mambo mengine.

Lakini pia unapaswa kuendelea kujikumbusha malengo yako makubwa, ili usipotee njia wakati unahangaika na mambo madogo madogo.
Mara kwa mara jikumbushe ndoto yako kubwa na jione ukiwa umeshaifikia na pata zile hisia ambazo utazipata pale utakapoyafikia.
Hili litakupa msukumo na uwazi wa kukuwezesha kusonga mbele ya kuzifikia ndoto zako kubwa.

Muhimu pia unapaswa kujitathmini kadiri unavyokwenda na pale inapokuwa muhimu kubadili mikakati unayofanyia kazi ili kuweza kufikia lengo.
Usiendelee tu kufanya kwa mazoea, badala yake tumia njia zilizo bora kuhakikisha unayafikia malengo yako makubwa.

Sheria ya leo; Kumbuka kwamba unachopaswa kufanyia kazi na kuzalisha matokeo ni malengo madogo madogo na siyo malengo makubwa ambayo hakuna unachofanya. Kuyagawa malengo makubwa kwenye vipande vidogo vidogo kutakusukuma kwenda kwenye uelekeo sahihi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#Ubunifu