2529; Mrefu halafu mfupi.
Kwenye ukurasa uliopita (2528), tumejifunza tamaa ya kutaka vingi kwa pamoja inavyokuwa kikwazo kwa wengi kufanya maamuzi.
Watu wanachelewa kufanya maamuzi kwa sababu hawataki kukosa fursa nzuri zinazoweza kujitokeza baadaye na hilo linakuwa kikwazo kwao.
Huo ni upande mmoja ambao watu wamekuwa wanatumia kukwepa kufanya maamuzi. Kwa sababu maamuzi yoyote yale yanaumiza kufanya, maana unapochagua kimoja, maana yake umekataa vingine.
Eneo jingine ambalo watu wamekuwa wanajificha ili wasifanye maamuzi ni kuwa na matakwa ambayo hayawezekani.
Yaani kujiwekea vigezo vya maamuzi ambavyo haviwezi kutokea kwa uhalisia.
Ni sawa na kusema unasubiri upate mtu ambaye ni mrefu halafu pia ni mfupi. Au mtu ambaye ni mwembamba na pia ni mnene.
Iko dhahiri kwamba mtu akishakuwa na sifa moja, hawezi tena kuwa na nyingine inayopingana na hiyo.
Hapo pamekuwa pazuri kujificha kwa sababu hakumsukumi mtu kufanya maamuzi na wala hakumpi majuto ya kwa nini haamui.
Kwa sababu ndani yake ana picha anayoitaka, picha isiyowezekana.
Mambo unayokuwa unataka hayatakuwa rahisi kama ufupi na urefu, bali yanakuwa magumu na yasiyoonekana kupingana wazi wazi.
Mfano umakuwa unataka mtu ambaye ni mchangamfu na ambaye ni msikivu na anayejali mambo yake.
Kiuhalisia kumpata mtu wa aina hiyo haiwezekani, kitendo tu cha mtu kuwa mchangamfu, tayari anajali sana mambo ya wengine.
Au unajiambia unataka biashara rahisi kufanya, inayolipa sana na isiyohitaji muda wako mwingi. Haishangazi kwa nini wenge mawazo ya aina hii huwa hawaanzi biashara, kwa sababu hicho wanachotaka hakipo. Biashara ilishakuwa inalipa sana, moja kwa moja itakuhitaji sana pia.
Hatua ya kuchukua;
Fikiria ni maamuzi gani ambayo umekuwa unachelewa kufanya kisha angalia vigezo ambavyo umejiwekea. Pitia kigezo kimoja kimoja kwa kulinganisha na vigezo vingine, utajionea wazi kwamba kuna vigezo ambavyo vinakinzana.
Bila kuondoa vigezo hivyo vinavyokinzana, hutaweza kufanya maamuzi.
Tafakari;
Huwa tunapenda kujificha bila kuonekana tumejificha. Kama hufanyi maamuzi na kuchukua hatua, angalia ni wapi ulipojificha. Kuwa na matakwa yasiyowezekana ni moja ya njia za kujificha usifanye maamuzi.
Kocha.