#SheriaYaLeo (33/366); Anachohitaji Menta.
Ili kujifunza kwa vitendo na uhalisia, unahitaji mtu ambaye tayari ameshafanikiwa kwenye kile unachotaka kufanikiwa ili awe menta wako.
Ni kupitia menta huyo ndiyo utajifunza kwa uzoefu ambao yeye ameupitia mpaka kufika alipofika. Atakusaidia kuepuka makosa ambayo yeye alifanya ili usijicheleweshe.
Ni muhimu sana kumpata aliyefanikiwa na awe tayari kuwa menta wako. Lakini hili siyo zoezi rahisi, kwa sababu waliofanikia wana mambo mengi tayari, hawawezi kumpa kila mtu nafasi.
Wengi wamekuwa wanakosa mamenta kwa sababu wanaenda kwa watu hao na shida zao tu, wakiomba wasaidiwe. Kwa njia hiyo watu hao waliofanikiwa huwa rahisi kukataa kwa kuwa hawana muda wa kumpa kila mtu.
Lakini hata watu hao ambao wamefanikiwa, kuna vitu wanahitaji, kuna changamoto wanakabiliana nazo.
Mtu anayeenda kwao akiwa na kile wanachohitaji au suluhisho la changamoto zao, wanakuwa kwenye nafasi kubwa ya kukubaliwa kuliko wanaoenda na shida zao tu.
Hivyo kwa yeyote unayetaka awe menta wako, tenga muda wa kujifunza kuhusu yeye na umjue kwa kina.
Jua mahitaji yake makuu au changamoto kubwa alizonazo.
Kisha nenda kwake uliwa na suluhisho linalomfaa, ukiwa na kitu chenye thamani kwake.
Ni kweli menta ana mengi ya kukupa, lakini unapoenda kwake na mahitaji yako tu, huwezi kumshawishi akupe nafasi.
Lakini unapoenda kwa menta ukiwa na majibu ya kile kinachomsumbua, unajiweka kwenye nafasi ya kukubaliwa.
Ni muhimu sana uwe na kitu cha kumpa menta wako kabla hujataka kupata kutoka kwake.
Sheria Ya Leo; Tafuta menta ambaye utajifunza kwa vitendo chini yake. Lakini badala ya kuangalia ni nini wanakupa pekee, angalia pia nini unawapa, vitu gani unaweza kuwasaidia. Hilo litakusaidia upate menta na mahusiano yenu yawe mazuri kwa sababu yana manufaa kwa wote.
#NidhamuUafilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu