2540; Umakini uliogawanyika.
Akili zetu zina uwezo mkubwa sana.
Lakini uwezo huo unaweza kufikiwa kama umakini wa akili utawekwa kwenye kitu kimoja kwa wakati.
Pale umakini wote unapowekwa kwenye kitu kimoja, uwezo wa akili unawezesha kifanyike kwa viwango vya juu sana.
Lakini pale umakini unapogawanyika, nguvu na uwezo wa akili unapungua na inashindwa kufanya makubwa.
Na hili unaweza kulifanyia jaribio wewe mwenyewe.
Tenga saa moja ya kusoma kitabu, halafu fanya hivyo katika hali mbili.
Hali ya kwanza zima simu yako au iweke mbali kabisa kwenye hiyo saa moja ya usomaji. Pia kaa eneo tulivu ambalo hakuna anayeweza kukusumbua. Weka umakini wako wote kwa saa nzima kwenye kusoma kitabu.
Hali ya pili kaa ni simu yako na soma huku pia ukiendelea kuchati na kuperuzi mitandao ya kijamii. Kwa saaa hiyo hiyo moja soma huku ukihangaika na mengine.
Kisha jifanyie tathmini, ni kwa urefu kiasi gani umeweza kusoma kwenye kila hali na uelewa wako upoje kwenye hali hizo mbili.
Fanya jaribio hilo na utajionea wewe mwenyewe jinsi umekuwa unafifisha uwezo mkubwa wa akili yako kwa kugawanya umakini wako.
Hatua ya kuchukua;
Fanya jaribio nililokushirikisha hapa na ujionee matokeo yake. Baada ya jaribio hilo, kila siku tenga muda ambao utakuwa unaweka umakini wako wote kwenye kile unachofanya na kutokuruhusu usumbufu wa aina yoyote ile. Hivyo ndivyo unavyoweza kufanya makubwa.
Tafakari;
Kipimo cha ufanisi siyo mengi kiasi gani umefanya, bali matokeo ya aina gani uliyozalisha. Unaweza kufanya mengi na kuchoka, lakini kusiwe na matokeo ya maana uliyozalisha. Ni bora kuweka umakini wako kwenye machache na kuyafanya vizuri, kuliko kuutawanya kwenye mengi na kuyafanya hovyo.
Kocha.
Asante kocha, kwenye Hili nimewahi kukufanya mara nyingi, pale unapoweka saa Moja ya kusoma bila kuingiliwa na usumbufu wowote unasoma kwa makini, unaongea na Nafsi Yako vyema kuhusiana na kile unachosema. Na unaweza kusoma kwa haraka zaidi.
Upande mwingine unaposoma huku unafanya vitu vingine huwezi kusoma kwa umakini na kuelewa kile unachosema. Unajikuta saa imeisha bila kuona cha maana ulichojifunza.
LikeLike
Vizuri kwa kuweza kuona tofauti hiyo, sasa linda sana umakini wako ili usigawanyike.
LikeLike