#SheriaYaLeo (45/366); Ufuate Ukinzani.

Sisi binadamu huwa tuna tabia ya kukimbia mambo ambayo ni magumu na yenye maumivu.
Tunapenda kufanya yale ambayo ni rahisi kwetu na yasiyoonyesha udhaifu wetu.
Kwa njia hii, tunashindwa kujijengea ubobezi, kwa sababu tunakuwa tumeweka nguvu na umakini wetu kwenye maeneo machache na ambayo ni rahisi kwetu.
Hii ndiyo njia wanayopita wengi wanaoishia kuwa wachanga, ambao hawafiki kwenye ubobezi.

Ili kufikia ubobezi, unapaswa kwenda njia ya tofauti, unapaswa kufuata ukinzani kwa kufanya mambo ambayo ni magumu na yenye maumivu.
Chochote ambacho ni muhimu kufanywa, ila wewe hupendi kukifanya, hicho ndiyo kinapaswa kuwa kipaumbele cha kwanza kwako.
Katika kufanyia hili kazi, kuna mambo mawili makubwa ya kuzingatia.

Moja ni kuacha kujihurumia. Lazima ujisukume wewe mwenyewe sana na lazima uwe mkosoaji wako mwenyewe. Acha kujidanganya kwamba uko vizuri na mambo yanakwenda vizuri. Kwa chochote unachofanya jua bado sana kufikia ubobezi, jua unapaswa kuwa bora zaidi ya ulivyo sasa.
Yaone madhaifu yako na yafanyie kazi ili yasiwe kikwazo kwako.
Ukabili kila aina ya ugumu unakutana nao badala ya kuukimbia.
Pata raha kwenye kuyavuka magumu unayokutana nayo, ili kuyaendea magumu makubwa zaidi na kujijengea ubobezi zaidi.

Mbili ni kukataa hadaa ya kulegeza umakini wako. Kadiri unavyokwenda, unapaswa kuongeza umakini na juhudi zako badala ya kupunguza.
Jiwekee viwango vya juu na pambana kufikia viwango hivyo kama ulivyojiwekea.
Usifike hatua ya kuona umeshajua hivyo huhitaji kuweka tena juhudi, badala yake endelea kukuza viwango vyako kadiri unavyokwenda.
Kwa kwenda hivi, utaweza kufikia ubobeza wa juu sana na wengine watashangaa jinsi inavyokuwa rahisi kwako kufanya makubwa, wasijue namna unavyojisukuma kwenye hilo.

Sheria ya leo; Jiwekee viwango vya juu sana kwenye kile unachofanya na unapokutana na magumu usiyakimbie, badala yake yakabili na uyavuke. Kila wakati jisukume kuvuka viwango ulivyojiwekea na kujiwekea viwango vipya. Na hapo ndipo utaweza kufikia ubobezi wa hali ya juu kabisa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu