2546; Kila kitu kina umuhimu.
Jambo moja kuhusu maisha ni kwamba kila kitu kina umuhimu.
Lakini kwa bahati mbaya sana, huwa hatuoni umuhimu wa kitu mpaka pale tunapokuwa tumeshakipoteza.
Unapokuwa na kitu unakizoea na kuona ubaya au madhaifu yake kuliko manufaa yake.
Ni mpaka pale unapokuwa umekipoteza ndiyo unaona jinsi kilivyokuwa na umuhimu.
Hata kama ni kitu unachoona kinakuumiza, bado kina umuhimu wake. Unayaona maumivu kwa sababu ndiyo unayoyaangalia zaidi. Utakapokikosa utaona mengine muhimu ambayo hukuwa unayaona awali.
Hii haimaanishi tuendelee kukubaliana na vitu hata kama havitufai, bali inatufundisha kutafuta mbadala wa kitu kabla ya kuachana nacho.
Kujua kina umuhimu gani na kuwa na mbadala wa kingine kinachotimiza umuhimu huo kabla ya kuachana nacho.
Hatua ya kuchukua;
Kwa kila kitu unachopanga kuachana nacho, jiulize kimekuwa na umuhimu gani, kisha pata mbadala kwenye umuhimu huo kabla hujaachana na kitu hicho. Hilo litakusaidia usikwame baada ya kuwa umeachana na kile ulichokichoka.
Tafakari;
Kubomoa ni rahisi, kujenga ni ngumu, kabla ya kubomoa chochote, hakikisha kuna mbadala uliojenga unaochukua nafasi ya unachobomoa. Sa sivyo utafurahia kubomoa kwa muda mfupi na kujutia kwa muda mrefu baada ya kukosa umuhimu wa kile ulichobomoa.
Kocha.