2555; Kuvunja mazoea kunahitaji kujali.

Ipo hadithi ya mwanamke ambaye alikuwa anakata mkia wa samaki kabla hajamkaanga.
Siku moja mume wake akamuuliza kwa nini anafanya hivyo, akamjibu ndivyo mama yake amekuwa anafanya.

Mume akamtaka wampigie simu mama yake kumuuliza. Walifanya hivyo na mama akajibu alikuwa anafanya hivyo kwa sababu ndivyo mama yake alikuwa akifanys.

Kwa bahati nzuri huyo bibi bado alikuwa hai, hivyo wakampigia simu kumuuliza kwa nini alikuwa anakata mkia wa samaki kabla ya kumkaanga.
Bibi alijibu alikuwa anafanya hivyo kwa sababu kikaangio chake kilikuwa kidogo, samaki hawakuwa wakienea kama asipowakata mkia.

Unaweza kuona hapo kitu kiliendelea kufanyika kwa vizazi viwili bila ya sababu yoyote. Yalikuwa tu ni mazoea ambayo watu wameshakuwa nayo na kuonekana ni sehemu ya maisha.

Kuna mambo mengi unayofanya kwenye maisha yako kwa mazoea ambayo hayana maana yoyote kabisa.
Unayafanya kwa uaminifu mkubwa, lakini hayana mchango wowote kwenye maisha yako.

Wakati mwingine unaweza kujua kabisa kwamba mambo hayo hayana maana, ila sasa kuyavunja au kuyapinga kunakuhitaji kazi kubwa ambayo haupo tayari kuiweka.

Kuvunja mazoea yoyote yale kunahitaji sana mtu uwe unajali.
Kwa sababu mazoea ni magumu kuvunja, hata kama hayana maana kabisa.

Hatua ya kuchukua;
Angalia ni mambo gani umekuwa unafanya kwa mazoea ila hayana manufaa yoyote kwenye maisha yako. Hayo ndiyo yanachukua muda na umakini wako na unashindwa kufanya makubwa.
Anza kujali kuhusu muda na umakini wako na kutoruhusu vipotee kwa namna yoyote ile.
Vunja mazoea yoyote ambayo hayana tija, hata kama yataleta ombwe fulani, utaliziba kwa yale unayopambana nayo kwenye safari yako ya mafanikio.

Tafakari;
Kama unafanys kitu leo kwa sababu ulikifanya jana,
Kama unafanya kitu kwa sababu ndivyo umekuwa unafanya,
Na kama unafanya kitu kwa sababu kila mtu anafanya,
Jua hapo upo kwenye mazoea.
Na mazoea yoyote hayawezi kukufikisha kwenye mafanikio makubwa.
Lazima uvunje kila aina ya mazoea ili kuweza kufanya makubwa.

Kocha.