2560; Kwa nini wewe.

Huwa ni rahisi kutumia kauli hii kulalamika pale mambo magumu yanapoonekana kukuandama wewe zaidi.

Labda ni magumu na changamoto unazokuwa umekutana nazo mara kwa mara na kudhani una kisirani, mkosi au bahati mbaya.

Tatizo ni kwamba, kila kitu kinachotokea unakihusisha zaidi na wewe, wakati vingi vimetokea kwa sababu ambayo haina uhusiano na wewe.

Chukua mfano ni siku umepanga kufanya kitu muhimu halafu mvua kubwa sana ikanyesha na ukashindwa kufanya kitu hicho kama ulivyopanga.

Unaweza kujiumiza kwa swali hilo la kwa nini wewe. Lakini mvua haiwajibiki kukuuliza wewe ni wakati gani inapaswa kunyesha au kutokunyesha.
Mvua inanyesha kwa ratiba zake yenyewe na siyo kuangalia matakwa yako.

Punguza kujiumiza na maswali haya ya kwa nini wewe, ili uweze kuweka juhudi sahihi kwenye maeneo sahihi na upate matokeo unayoyataka.

Hatua ya kuchukua;
Kila mara unapojiambia kwa nini wewe kutokana na jambo lililotokea, jiulize kwanza kama ni kitu kilicho ndani ya uwezo wako kukiathiri. Kama ni kitu kipo ndani ya uwezo wako, unapaswa kuchukua hatua kukitatua. Kama kipo nje ya uwezo wako, hupaswi kuhangaika nacho kwa sababu huwezi kukiathiri.

Tafakari;
Kama dunia ingekuwa inamsikiliza kila mtu ndiyo ifanye mambo yake, ingechanganyikiwa kabisa. Maana wakati wewe unataka mvua, kuna wenzako wanataka jua. Na wakati wewe unataka jua, wenzako wanataka mvua.
Dunia inaenda kwa mambo yake na sisi ndiyo tunapaswa kubadilika kuweza kwenda nayo na siyo kutegemea dunia iende kwa matakwa yetu.

Kocha.