2561; Msitu na mti.
Ukiwa mbali na ukauangalia msitu, unakuwa ni wa kupendeza kabisa.
Kijani kimekuwa kinatawala na utadhani miti yote iko sawa.
Ukiingia ndani ya msitu huo, ule ukijani mzuri uliokuwa unauona kwa mbali huuobi tena.
Bali unaanza kuona mti mmoja mmoja na unagundua siyo miti yote iko vizuri.
Kuna iliyopinda, ipo inayokauka na kuna iliyovunjika.
Unaweza kudhani umedanganywa au kuhadaiwa, iweje kwa mbali uone kila kitu kipo vizuri halafu kwa karibu uone kuna ambavyo havipo sawa?
Hivyo ndivyo maisha yalivyo kwenye kila eneo, kwa mbali kila kitu ni kizuri, ni mpaka usogee karibu ndiyo utaweza kuziona changamoto zilizopo.
Ndiyo maana biashara huonekana nzuri sana kabla hujaingia, ila unapoingia ndiyo unakutana na changamoto ambazo hukujua zipo.
Ndiyo maana kazi inaonekana nzuri sana kabla hujaipata, ukishaipata na kuifanya kwa muda ndiyo unagundua matatizo yaliyo ndani yake.
Hata watu, kabla hujawa nao karibu unaona wako vizuri kabisa, hawana matatizo yoyote. Ni mpaka unapokuwa nao karibu ndiyo unayajua madhaifu yao ambayo yanaleta matatizo mbalimbali.
Hatua ya kuchukua;
Unapopanga kuingia kwenye kitu chochote kipya, jikumbushe kwamba kuna vitu vya ndani ambavyo hujui kuhusu kitu hicho. Hivyo kuwa tayari kujifunza na kuchukua hatua sahihi.
Ukiingia kwenye kitu kwa kuona mazuri yake tu na kudhani mazuri hayo ndiyo yaliyopo pekee unajidanganya na unajiandaa kwa maumivu makali.
Tafakari;
Hukijui kitu kama bado hujaingia ndani na kukifanya. Haijalishi umejifunza na kutafiti kwa kiasi gani, unapoingia ndani kuna vipya utaviona ambavyo kwa nje vilikuwa havionekani.
Kocha.
Ni kweli kabisa kocha, kwa mbali vitu vinaonekana
Vizuri lakini unapoingia ndani unagundua kuwa kumbe kuna matatizo ambayo huyaoni.
LikeLike
Hakika.
LikeLike