#SheriaYaLeo (66/366); Zawadi ya akili yetu halisi.
Wote tunamiliki nguvu kubwa ya ubunifu tuliyozaliwa nayo na inayotaka kujidhihirisha.
Hiyo ni zawadi ya akili yetu halisi, ambayo ina uwezo mkubwa sana.
Akili ya binadamu kwa asili ina ubunifu mkubwa ndani yake. Kila wakati ikitafuta njia za kujenga uhusiano na muunganiko baina ya vitu na mawazo.
Akili huwa inataka kuchunguza na kugundua vitu vipya kuhusu dunia na kuja na uvumbuzi mpya.
Kuonyesha nguvu hiyo ya ubunifu ndiyo hitaji letu kubwa wanadamu. Na kulipuuza hitaji hilo ndiyo chanzo cha ukawaida na matatizo.
Kinachoua nguvu yetu ya ubunifu siyo uzee au kukosa kipaji, bali nafsi zetu na mtazamo tunaokuwa nao.
Tunakuwa tumezoea na kufarijika sana na ujuzi na maarifa tuliyonayo.
Tunahofia kujifunza na kujaribu vitu vipya kwa sababu hatuna uhakika navyo na vina hatari kubwa.
Tunaona ni bora kupata matokeo madogo tuliyozoea na ya uhakika, kuliko kujaribu mambo mapya ambayo yanaweza kuleta matokeo makubwa, lakini pia yana hatari ya kushindwa.
Kuhofia kushindwa na kuchekwa pale mtu unaposhindwa ndiyo kitu kinachoua ubunifu ulio ndani yetu, kutuweka kwenye mazoea na kutuzuia tusifikie ubobezi wa juu zaidi.
Sheria ya leo; Fanya kile ambacho akili inataka kufanya – karibisha, kumbatia na fanyia kazi mawazo mapya.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu