#SheriaYaLeo (68/366); Baki na udadisi wako.
Wakati unaanza safari ya ubobezi, unakuwa na udadisi mkubwa, kitu kinachokusukuma kujifunza mambo mengi na kuweza kufanya mapya na makubwa.
Hilo linapelekea upate matokeo mazuri.
Na hapo ndipo hatari inapoanzia.
Kutokana na matokeo mazuri unayokuwa umepata, unaacha kuwa mdadisi, unajiona umeshajua kila kitu na hilo linakufanya ubaki kwenye mazoea.
Unaacha kuuliza maswali uliyokuwa unauliza mwanzo na kuacha kujifunza vitu vipya, kwa kujiona tayari una majibu yote, tayari unajua kila kitu.
Hali hiyo inazuia akili isiweze kukua na mtu kushindwa kupata matokeo makubwa zaidi.
Ubunifu unashuka na mtu anaanguka kutoka kwenye ubobezi na mafanikio anayokuwa amefikia.
Unapaswa kupambana na hali hii, kwa kuendelea kubaki na udadisi wako na kuendelea kujikumbusha vitu vingi sana ambavyo bado hujui.
Jikumbushe hata kama unaona unajua kiasi gani, unachojua ni tone tu kwenye bahari ya yale unayojua.
Kadiri unavyoendelea kujifunza, ona jinsi ambavyo hujui mengi zaidi.
Hilo likusukume kuendelea kujifunza na kujaribu mambo mapya, kitu kitakachokufanya uwendelee kuwa mbunifu na ufike na kubaki kwenye ubobezi wa juu.
Sheria Ya Leo; Asili ina miujiza isiyo na mwisho. Iruhusu asili iendelee kukushangaza kwa wewe kuwa na udadisi. Kila mara jikumbushe jinsi ambavyo kuna mengi ambayo bado hujayajua.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu