#SheriaYaLeo (69/366); Kukosa uvumilivu ni adui mkubwa.

Kikwazo kikubwa zaidi kwenye ubunifu wako ni kukosa uvumilivu.
Ile hali ya kuharakisha na kutaka kupata matokeo makubwa kwa haraka ni kikwazo kikubwa kwako kufikia ubobezi wa hali ya juu.

Unapoharakisha, hupati muda wa kujifunza kwa kina na kubobea yale ya msingi kwenye kile unachofanya.
Kwa haraka zako unaweza kudhani una ubunifu kubwa unaiga tu mitindo ya wengine.
Hakuna chochote kipya na cha kipekee unachokuwa umeweka kwenye kile unachofanya.

Wale unaowalenga siyo wajinga, wanajua wazi kama kweli mtu unajua na umebobea kwenye kile unachofanya au unafanya tu kwa juu juu.
Wakishajua hujali kweli kile unachofanya na unaharakisha tu ili kupata unachotaka, hawataendelea kuwa na wewe, badala yake watakuacha.

Njia bora kabisa ni kupenda kujifunza na kujipa muda wa kutosha kwenye kujifunza.
Mtu yeyote atakayeweka miaka kumi kujifunza kwa kina, kujaribu vitu vipya na kujenga ubobezi, lazima atajikuta anatengeneza sauti ya kipekee kwake ambayo inawavutia wengi kwake.
Hilo halitokei kwa bahati au upendeleo, bali kwa kujipa muda na kuwa na uvumilivu.

Sheria Ya Leo; Kuwa na mtazamo wa muda mrefu. Kwa kuwa mvumilivu na kufuata mchakato, upekee wako utajidhihirisha wenyewe na utaweza kuwa na ubunifu mkubwa na kufikia ubobezi wa hali ya juu.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu