2566; Vichache na vingi.
Kwenye zama tunazoishi sasa, kuna mambo mengi sana ya kufanya.
Na unaweza kufanya karibu kila kitu.
Hebu angalia tu biashara zinazofanyika kwenye eneo ulilopo, karibu zote unaweza kuzifanya.
Na wakati mwingine unajiambia kabisa, yaani hawa wanaweza hivi, hata mimi siwezi kushindwa.
Hilo linaweza kukushawishi uhangaike na mambo mengi, kwa kuona unachangamkia fursa zilizopo.
Tatizo kubwa linakuja kwamba unahangaika na mambo mengi, huku machache tu yakiwa yamekushinda.
Sasa kama machache tu yamekushinda, utayawezaje mengi?
Ni vyema uweze kuyafanya vizuri kabisa machache uliyonayo, kabla hujayakimbilia mengi.
Maana kuweza kufanya na kufanya kwa uhalisia ni vitu viwili tofauti.
Hatua ya kuchukua;
Orodhesha mambo yote unayoona unaweza kufanya na unatamani uanze kuyafanya.
Kabla hujayaanza hayo, hakikisha kwanza machache unayofanya sasa unayafanya vizuri kabisa, kwa viwango vya juu na hayawi changamoto au kikwazo kwako.
Ukishayaweza vizuri machache, ndiyo unaweza kwenda kwenye mengi.
Tafakari;
Ni bora kufanya machache kwa ubora wa hali ya juu kabisa kuliko kufanya mengi kwa hovyo.
Maana mafanikio hayapo kwenye wingi wa unayofanya, bali yapo kwenye ubora wa unayofanya.
Kocha.