2569; Kuadhibiwa na unachokitaka.

Werevu wamewahi kusema ukitaka kumwadhibu mtu, mpe kile anachokitaka, tena kwa namna anavyokitaka.

Ni kauli ambayo wengi huwa hawaielewi, ila twende kwenye mifano tuweze kujionea uhalisia wake.

Chukua mtu anayecheza bahati nasibu, wote tunajua anataka ushindi. Sasa chukua mtu aliyeshinda bahati nasibu, baada ya muda maisha yake huwa ni ya hovyo kuliko yalivyokuwa kabla hajashinda bahati nasibu hiyo.

Angalia pia upande wa umaarufu, kabla mtu hajapata umaarufu anaweza kuutafuta kwa kila hali. Lakini akishaupata umaarufu ndiyo anajua changamoto zake na kutamani asingefikia kwenye umaarufu huo.

Hilo pia lipo kwenye utajiri, kuna wengi ambao wanaanzia chini, wakiwa na hamu kubwa ya kufikia utajiri. Wanakuwa na nidhamu kubwa ya kupambania hilo na wanalifikia. Baada ya kufikia utajiri mambo yanabadilika kabisa, wanajikuta wakisumbuka sana na hata baadaye kuanguka kabisa.

Ni kama kuna laana fulani hivi, kwamba kadiri unavyokitaka sana kitu, ndivyo unapokipata kinakuwa maumivu na adhabu kubwa kwako.

Je hili linamaanisha tusitake kupata vitu fulani?
Majibu ni hapana, tunapaswa kutaka vitu mbalimbali, lakini hatupaswi kuweka matumaini yetu yote kwenye kupata kitu hicho.
Kwani matumaini yetu yanapokuwa kwenye matokeo na tukafikia matokeo hayo, tunakuwa hatuna tena matumaini.
Na hakuna kitu kibaya kama maisha yasiyokuwa na matumaini. Ni maisha hatari na huishia kwenye uharibifu.

Haijalishi upo kwenye hatua ipi ya maisha, unapaswa kuwa na tumaini endelevu ambalo utakuwa unafanyia kazi kila wakati.
Na hapo ndiyo muhimu sana kulijua kusudi la maisha yako na kuliishi, kwani hilo ndiyo litakupa tumaini endelevu.
Kusudi la maisha huwa halifiki mwisho mpaka pale unapokufa.

Hatua ya kuchukua;
Kila wakati jiulize ni tumaini gani unalo. Kama huna tumaini jua upo hatarini kuyapoteza maisha yako. Jua na ishi kusudi lako ili kuwa na tumaini endelevu.

Tafakari;
Tumaini ndiyo injini ya maisha ya kila mtu. Pale tumaini linapokosekana, maisha huwa hovyo na kuharibika kabisa. Mara zote kuwa na tumaini ili maisha yawe kwenye mkondo mzuri.

Kocha.