2570; Rahisi ni ghali, mbaya na ngumu.

Unapokuwa njia panda na hajui njia ipi uchukue kati ya njia zilizo mbele yako, kama kuna njia rahisi na ngumu, mara zote chukua njia ngumu.

Kwenye safari ya mafanikio, rahisi ni ghali, mbaya na ngumu.
Rahisi ni ghali kwa sababu haina ubora mkubwa, hivyo hata kama utanunua kwa bei rahisi, utaishia kununua mara nyingi kuliko anayenunua ghali.

Rahisi ni mbaya kwa sababu kwa urahisi wake, juhudi na umakini mkubwa haviwekwi na hilo hufanya matokeo yawe ya kawaida, ambayo kwa lugha nyingine ni mabaya.

Na rahisi ni ngumu kwa sababu kila mru anapenda rahisi, hivyo ushindani huwa mkubwa sana na hilo kuleta ugumu.

Kwa asili sisi binadamu tunapenda urahisi, hivyo ili kuuepuka ni lazima uweke juhudi za makusudi.
Kundi kubwa linalokimbilia kwenye urahisi lina ushawishi mkubwa kwako na wewe ukae kwenye urahisi huo waliopo wengi.
Lakini mara zote jikumbushe kuhangaika na urahisi hakujawahi kumpa yeyote mafanikio makubwa.
Usijidanganye wewe utakuwa wa kwanza kivunja hilo.

Hatua ya kuchukua;
Fikiria mara zote kwenye maisha yako ambazo umekimbilia kufanya mambo rahisi kwenye maisha yako. Angalia mambo hayo rahisi yaliishaje. Mengi yaliisha kirahisi kama yalivyokuwa kiurahisi.
Acha kukimbizana na urahisi badala yake kimbizana na usahihi.

Tafakari;
Kitu kilishakuwa rahisi, kila mtu anakimbilia kukifanya, ushindani unakuwa mkubwa na faida inakuwa ndogo pia.
Na hivyo ndivyo maisha yalivyo kwenye maeneo mengi, kila unapochagua kitu kimoja, unakuwa umekosa kitu kingine.
Jua kabisa wapi unataka kufika ili uweze kufanya maamuzi sahihi.

Kocha.