2572; Kipi kingine unachojali zaidi?

Kile unachokijali zaidi, ndiyo unachokipa umakini wako na hicho ndiyo kinachokua zaidi.

Kama una ndoto kubwa ambazo ndiyo unazijali zaidi, fikra zako zote zinakuwa kwenye ndoto hizo na mengine yote unayapuuza.

Kila wakati unakuwa unapambana na namna ya kufikia ndoto ulizonazo na hicho tu ndiyo unachojali.

Hupati muda wa kujali vitu vingine nje ya ndoto hizo.
Hupati muda wa kufikiria wengine wanakuchukuliaje.
Wewe kipaumbele chako ni ndoto zako kubwa, mengine unayapuuza.

Bilionea na mwekezaji Peter Thiel, ambaye amewekeza kwenye makampuni mengi ya teknolojia tangu yakiwa machanga ni mmoja wa watu wachache ambao wamekuwa wanaweza kuona vipaji vya tofauti mapema sana.

Na anasema kwa uzoefu wake kwenye eneo la teknolojia, wanaofanikiwa sana ni wale ambao wana tatizo fulani la kiakili linalowafanya wasijali wengine wanawachukuliaje. Kwa tatizo hilo la akili, wanakuwa tayari kufanyia kazi mawazo yao, hata kama wengine watawabeza na kuwacheka au kuwasema vibaya, hawajali.
Wakati wengine wanaangalia wengine wanafanya na kusema nini na wakaiga, wao wanakomaa na kile walichochagua, hata kama wako peke yao.

Mwisho wa siku hao ndiyo wanaopata mafanikio makubwa.
Yote hiyo inaanzia kwenye kujali zaidi kile wanachofanya na kupuuza mengine yote.

Sasa rafiki, ukishajiona unajali sana wengine wanakuchukuliaje au kusemaje kuhusu wewe. Ukishajiona unafanya vitu ambavyo roho yako haitaki ila tu unataka kuwaridhisha wengine. Jua kabisa kuyafikia mafanikio makubwa ni kitu kigumu sana kwako.
Kwa sababu unayohangaika nayo ni kikwazo kikubwa kwako kufanikiwa.

Mafanikio makubwa yanataka akili yako yote na umakini wako wote uwe kwenye kile unachotaka kufikia na siyo kusumbuka na mambo mengine.

Hatua ya kuchukua;
Jiangalie wewe mwenyewe ni mambo gani umekuwa unayajali zaidi. Je kati ya ndoto yako kubwa na mambo mengine, kipi kipaumbele kikubwa zaidi kwako.
Kama kuna kitu kingine chenye kipaumbele kikubwa kuliko ndoto zako, jua safari ya kuzifikia ndoto hizo itakuwa ngumu sana kwako.

Tafakari;
Kipimo rahisi cha kama umejitoa kweli kwa ndoto ulizonazo na kama utazifikia ni namna unavyojali kuhusu mambo mengine.
Kama kuna vitu unavipa kipaumbele kikubwa kuliko ndoto zako, usijidanganye, safari ya kuzifikia itakuwa ngumu sana.

Kocha.