#SheriaYaLeo (82/366); Fanya Tahajudi.

Safari ya ubobezi na kuelekea kwenye mafanikio makubwa inahitaji ukomavu, utulivu na umakini wa muda mrefu.

Wengi huanza safari hiyo wakiwa na hamasa ya hali ya juu sana.
Lakini kadiri muda unavyokwenda hamasa hiyo inapoa na wanajikuta wakirudi kwenye mazoea.

Mawazo yao yanahama hama na hayawezi kukaa kwenye kile walichochagua kufanyia kazi kwa muda mrefu.

Usumbufu wa nje nao unavuruga utulivu wao na kuwaondoa kwenye kile wanachopaswa kukipa umakini mkubwa.

Hivyo ndiyo safari ya ubobezi kwa wengi inavyofika ukingoni na kujikuta kila mara wanarudi kwenye mazoea yao.

Kuepuka njia hiyo unapaswa kuwa unafanya tahajudi (meditation).
Lengo la tahajudi hiyo ni kutuliza fikra zako na kukuwezesha kuweka umakini wako kwenye kitu kimoja kwa muda mrefu.

Tahajudi pia inakupa ukomavu wa kuweza kuvuka changamoto ambazo kwa wengine zingeweza kuwa kikwazo kikubwa.

Jiwekee utararibu wa kufanya tahajudi kila siku asubuhi ili uweze kupata manufaa yake ambayo yatakuwezesha kuendelea na safari ya ubobezi bila kuishia njiani.

Sheria ya leo; Ili kufikia ubobezi, akili yako lazima iweze kutulia kwenye kitu kimoja kwa muda mrefu bila kuchoka au kuhama. Tumia tahajudi kuijengea akili yako uwezo huo.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji