2579; Mpaka uelewe.
Upo usemi wa Kiswahili kwamba asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu.
Unaweza kupata maana mbalimbali kwenye usemi huo, lakini kuna maana moja nimeona ina nguvu kubwa sana.
Iko hivi, mtoto anapokosea, mzazi humwadhibu.
Kama mtoto ataendelea kukosea, mzazi hawezi kuendelea kumwadhibu, atafika mahali na kumwonea huruma.
Na hapo sasa ndipo mtoto huyo anajifunza kumbe anaweza kukosea na maisha yakaenda tu.
Atakachokuja kujifunza kwa maumivu makali ni kwamba dunia haina huruma kama mzazi.
Ukikosea dunia itaendelea kukuadhibu mpaka uelewe.
Dunia haijali kabisa imekuadhibu mara ngapi, haijali utakuwa sugu, haijali utaumia au kufa.
Yenyewe ina sharti moja tu, akikosea adhibu.
Hatua ya kuchukua;
Ni adhabu gani imekuwa inajirudia mara kwa mara kwenye maisha yako? Hicho ni kiashiria kwamba kuna somo hujalielewa na dunia itaendelea kukuadhibu mpaka uelewe.
Kipato kidogo kuwa endelevu ni adhabu ambayo dunia inakupa kwa kutokutoa thamani.
Kudharauliwa na wengine ni adhabu ambayo dunia inakupa kwa kutokujiheshimu mwenyewe.
Chochote kinachokusumbua, ni dunia inakuadhibu kwa kitu fulani ambacho hujaelewa na adhabu hiyo itakwenda mpaka utakapoelewa.
Tafakari;
Dunia ni shule, maisha ni darasa. Kutoka darasa moja kwenda jingine kuna mtihani na huwezi kuvuka darasa bila kufaulu mtihani huo. Utaendelea kurudia mtihani mpaka utakapoufaulu. Dunia haina huruma kwamba itakupitisha kwa kuwa umerudia mara nyingi. Inataka uelewe kitu kwa kina ndiyo uweze kupiga hatua.
Kocha.