#SheriaYaLeo (83/366); Sikiliza Kuvurugwa Kwako.

Kwa chochote unachofanya, huwa unaanza na hamasa na msukumo mkubwa, ambao unakuwezesha kufanya kitu hicho kwa muda bila kuchoka.

Lakini baada ya muda unajikuta kwenye hali ya kuvurugwa, ambapo unakutana na mkwamo mkubwa na ugumu mkubwa wa kuendelea.

Huo ndiyo wakati wenye fursa nzuri, kwa sababu unakupa nafasi ya kurudi nyuma na kuangalia kwa kina kile unachofanya ili kuweza kuja na ubunifu mpya na wa kipekee.

Unapopitia wakati kama huo, usikate tamaa na kuona kama ndiyo mwisho, badala yake iondoe akili yako kwenye jambo hilo kwa muda.
Fanya matembezi au jipumzishe kwa muda na bila ya kujua utashangaa suluhisho linaluja lenyewe kwenye akili yako.

Unapokutana na ugumu au kuvurugwa ni fursa nzuri kwako kupitia kile unachofanya na kuja na njia tofauti ya kukifanya inayoleta matokeo bora zaidi.

Sheria ya leo; Unapojikuta kwenye mkwamo kwa kile unachofanya, iondoe akili yako kwa muda, nenda ukatembee au fanya kitu kingine cha tofauti. Ubongo wako utakurudisha kwenye kitu hicho ukiwa na njia bora zaidi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji