Rafiki yangu mpendwa,

Watu wengi wanaofundisha kwenye tasnia ya maendeleo binafsi kuwa wanaipa ajira picha mbaya.
Kwamba ni utumwa wa kujitakia na ambao ni mbaya kabisa.

Japo hilo lina ukweli kwa wengi, hasa kwa namna wanavyokuwa wameizoea na kuitegemea ajira, kwa wachache siyo sahihi.
Kuna wachache ambao wamekuwa wanatumia ajira kama njia ya kufika kwenye ndoto zao kubwa.

Kama upo kwenye ajira, kaa hapa kwa utulivu kwani naenda kukuonyesha jinsi ya kuwa sehemu ya hao wachache.

Kuna sababu kubwa mbili tu ambazo zinapaswa kufanya mtu kuajiriwa. Nje ya sababu hizo mbili ajira inageuka kuwa utumwa ambao unamtesa sana mtu.

Hapa unakwenda kujifunza sababu hizo mbili na jinsi ya kuzijenga kwako mwenyewe ili ajira iwe na manufaa kwako.

Sababu ya kwanza ni kujenga mtaji.

Ajira ina kipato chenye ukomo, ambacho peke yake hakiwezi kukufikisha kwenye utajiri na uhuru wa kifedha.

Hata uwe unalipwa mshahara mkubwa kiasi gani, peke yake hauwezi kukupa utajiri mkubwa.

Kinachokupa utajiri ni mtaji unaoujenga kupitia ajira na kisha kuuwekeza vyema, kwa kuanzisha biashara au kufanya uwekezaji kwenye maeneo mbalimbali kama ardhi, majengo na masoko ya mitaji.

Hatua ya kuchukua;
Itumie ajira yako kama sehemu ya kujenga mtaji.
Unapopokea mshahara usiutumie wote, hata kama ni mdogo kiasi gani.

Tenga fungu kwenye kila mshahara wako na liweke kwenye akiba ambayo huwezi kuitumia.
Kuwa na akaunti maalumu ya kuweka akiba hiyo, ambayo unaweza kuweka ila huwezi kutoa.

Na pia kuwa na mpango wako wa uwekezaji, wapi unawekeza mtaji unaokusanya ili uweze kukuzalishia faida, kukua thamani na kuwa salama.

Sababu ya pili ni kujenga ujuzi na uzoefu.

Kama una lengo la kuingia kwenye biashara ya aina yoyote ile, ujuzi na uzoefu ni mtaji muhimu sana kuwa nao.

Lakini kwa wengi mtaji huo wanakuwa hawana. Hivyo wanapoingia wanaishia kupoteza vibaya.

Unaweza kutumia ajira kama njia ya kujenga ujuzi na uzoefu ambao utaweza kuutumia pale unapofungua biashara yako.

Mfano kama unataka kuanzisha biashara ya saluni, itakuwa vyema kama utafanya kazi kwa muda kwenye saluni ya mtu mwingine.

Hilo linakupa fursa ya kujifunza na hata kufanya makosa kwenye biashara ya mwingine kabla ya kwenda kuanzisha biashara yako mwenyewe.

Ujuzi na uzoefu unakupa mwongozo wa vitu gani vya kufanya na vipi vya kuepuka ili kufanikiwa kwenye biashara husika.

Hatua ya kuchukua;
Jiulize ni ujuzi na uzoefu gani unaojijengea kwenye ajira uliyopo.
Kisha jiulize ni jinsi gani unaweza kutumia ujuzi na uzoefu huo kujiingizia kipato nje ya ajira hiyo.

Hata kama ni kupitia kutoa mafunzo au ushauri kwa wengine, itakuwa ni manufaa makubwa kutoka kwenye ajira hiyo.

Rafiki, hizo ndizo sababu mbili za msingi kabisa kwa mtu kuwa kwenye ajira.
Sababu nyingine yoyote nje ya hizo mbili ni utumwa tu wa kujitakia.

Mfano mtu anapokuwa kwenye ajira kwa sababu ya kipato cha uhakika, huu ni utumwa kwa sababu maisha yako yote yanategemea chanzo kimoja tu, jambo ambalo ni hatari.

Au mtu anapokuwa kwenye ajira kwa sababu ataweza kukopesheka, ni utumwa kwa sababu mikopo ina riba kubwa na ni vigumu kuweza kuitumia vizuri ukiwa kwenye ajira.

Sababu nyingine ya kitumwa ni kutaka kuonekana mtu wa hadhi fulani. Kama hadhi yako umeishikiza kwenye ajira uliyonayo, hutaweza kujiamini wewe mwenyewe.

Rafiki yangu mpendwa, kuweza kutumia ajira kama daraja zuri la kukufikisha kwenye ndoto zako kubwa, hakikisha unasoma kitabu cha BIASHARA NDANI YA AJIRA.

Kitabu hicho kitakupa maarifa ya kukuwezesha kuanzisha na kukuza biashara yako ukiwa bado umeajiriwa.
Utajifunza kuepuka makosa ambayo umekuwa unafanya unapojaribu kuanza biashara ukiwa kwenye ajira na zikaishia kufa.

Wasiliana sasa na 0752 977 170 kujipatia nakala yako ya kitabu cha BIASHARA NDANI YA AJIRA ili uweze kuitumia ajira kama daraja sahihi kwako kufikia ndoto zako kubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Muuza Matumaini, Kocha Dr. Makirita Amani.